CHADEMA WAIPASUA CCM SHINYANGA, WAMCHOMOA KATIBU MWENEZI WILAYA, DIWANI VITI MAALUM.
Charles shigino akiongea na waandishi wa habari mjini shinyanga
katibu wa muenezi wa ccm wilaya ya shinyanga charles shigino
KATIKA
hali isiyokuwa ya kawaida, katibu wa siasa na uenezi wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) wilaya ya Shinyanga mjini, Charles Shigino ametangaza rasmi kukihama
chama chake cha CCM na kujiunga na CHADEMA.
Shigino
ambaye pia alikuwa mmoja wa wana CCM walioomba kugombea ubunge kwa tiketi ya
CCM jimbo la Shinyanga ametangaza uamuzi
wake huo mbele ya waandishi wa habari na kueleza kuwa moja ya sababu
iliyosababisha achukue uamuzi huo ni kuchoshwa na mizengwe iliyomo ndani ya
chama hicho.
Alisema
ndani ya Chama cha Mapinduzi mambo mengi yamekuwa hayaendeshwi kwa mujibu wa
katiba na taratibu za chama na badala yake kufuata matakwa ya watu binafsi
ikiwemo kukithiri kwa vitendo vya rushwa hali inayokidhalilisha chama hicho.
“Mimi
ni miongoni mwa wana CCM tulioomba kugombea nafasi ya ubunge ndani ya Chama
chetu, lakini mizengwe inayoendelea inayofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM nimeona hata
kama nikishinda kura za maoni kuna mipango ya jina langu kukatwa kutokana
na chuki binafsi,”
“Pamoja
na kuwa kiongozi wa kiwilaya lakini nimekuwa sishirikishwi kwenye vikao vingi
vya kikatiba, mara nyingi ninapotetea haki za wananchi wetu naelezwa eti mimi
ni msaliti, sasa nimechoka na nimeamua kubwaga manyanga na nimetangaza kujiunga
na CHADEMA,” alieleza Shigino.
Kaimu
katibu wa CHADEMA wilayani Shinyanga, George Kitalama amethibitisha kupokelewa
rasmi kwa mwenezi huyo wa CCM na kwamba alikabidhiwa kadi ya CHADEMA juzi
pamoja na aliyekuwa diwani wa viti maalum (CCM) kata Ibadakuli Zimila Kalwani.
Kitalama
alisema ndani ya kipindi cha wiki nzima CHADEMA imepokea zaidi ya wanachama 400
kutoka CCM waliojiunga na chama hicho na kwamba hali hiyo inatokana na wana CCM
hao kuchoshwa na mfumo mbovu uliomo ndani ya chama hicho.
“Ni
kweli jana tumempokea rasmi katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini
tangu jana (juzi), na siyo yeye tu kwa siku mbili za juzi na jana tumepokea
wana CCM 36 na mpaka sasa tuna zaidi ya wanachama 400 waliojiunga na CHADEMA
wakitokea CCM, ni hatua nzuri kwetu wakati tukielekea kwenye uchaguzi mkuu,”
alieleza Kitalama.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini, Kanali mstaafu Tajiri
Maulid alisema hakuwa na taarifa juu ya mwenezi wake kuhamia CHADEMA na kwamba
ofisi yake pia haijapata taarifa rasmi juu ya tukio hilo.
“Sina
taarifa kama kweli huyo bwana amekimbilia CHADEMA, ndiyo kwanza
nasikia kutoka kwako, na kama ni kweli itakuwa nafuu kwetu, maana
alikuwa mzigo, tunashukuru kwa kuondoka kwake, na ndiyo maana leo
hii (jana) hakuongozana na wagombea wenzake kwenye mikutano ya kuomba
kura kwa
wana CCM kwa ajili ya kura za maoni,” alieleza Kanali Maulidi.
Kwa
kipindi kirefu Shigino alikuwa haelewani na viongozi wenzake ndani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) ambapo aliwahi kusimamishwa uongozi kwa madai ya kukiuka kanuni
za chama kutokana na kitendo chake cha kuwatetea wafanyabiashara wadogo
(machinga) waache kufukuzwa ovyo mitaani.
No comments: