Majambazi sita wameuawa kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za miili yao na Jeshi la Polisi baada ya kutokea majibizano ya risasi kati ya polisi na majambazi hao na kupatikana silaha moja aina ya AK 47 na nyingine nne zilizotengenezwa kienyeji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Ahmed Msangi amesema tukio hilo limetokea usiku wa Julai 8, 2017, katika mtaa wa Fumagila mashariki kata ya Igoma wilaya ya Ngamagana mkoani Mwanza baada ya kupokea taarifa kwa kwamba baadhi ya watu wanaofanya uhalifu katika mkoa wa Pwani wilaya ya Kibiti na Rufiji wamekimbilia mkoani humo wakijipanga kutengeneza vikundi vya kufanya uhalifu.
Kamanda Msangi amesema katika ufuatiliaji walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye katika mahojiano alikiri kuhusika na tukio la unyang’anyi kwa kutumia silaha, kisha alitoa ushirikiano kwa askari ambapo aliwapeleka hadi eneo la Fumagila ambapo alidai wenzake wamejificha eneo hilo, ghafla majambazi hao walikurupuka na kuanza kuwarushia askari polisi risasi.
Aidha, kutokana na umahiri wa askari hao waliweza kujibu mashambulizi na kufanikiwa kuwauwa majambazi sita huku wengine wawili wakifanikiwa kutoroka eneo la tukio lakini polisi walifanikiwa kukamata silaha kadhaa na vitu vingine.
Pamoja na hayo, DCP Msangi amesema hakuna askari aliyejeruhiwa kwa risasi wala kupoteza maisha katika tukio hilo huku akisisitiza kuwa ufuatiliaji wa kusaka na kuwatia nguvuni waliotoroka bado unaendelea.
Shuhuda wa tukio hilo, ambaye ni diwani wa Kata ya Kishili iliyo jirani na kata hiyo, Sospeter Ndumi amesema kurushiana risasi baina ya watu hao na polisi kulianza usiku wa manane hadi majira ya jana asubuhi.
Amesema katika majibizano hayo polisi walifanikiwa kuwaua watu hao na kukamata silaha mbalimbali za kivita walizokuwa wanazitumia.
Katika mtaa huo huo ndipo lilipotokea tukio la Desemba 3 mwaka jana ambapo polisi waliwakamata watoto 11 wenye umri unaokadiriwa kuwa na miaka sita hadi 14 baada ya kuizingira nyumba moja kwa lengo la kuwakamata watu waliowahisi kuwa majambazi.
Mmoja kati ya watu watatu waliokutwa kwenye nyumba hiyo alikimbia baada ya kuwarushia polisi bumu la mkono, kabla ya polisi kuwadhibiti waliosalia kwa kushirikiana na wananchi wa mtaa huo.
Kadhalika katika tukio hilo, watu watatu waliosadikiwa kuwa ni majambazi waliuawa na bunduki mbili aina ya SMG na AK47, magazine saba, bastola moja na risasi 183 vilikamatwa na polisi.
Baada ya polisi kuondoka katika eneo hilo, wananchi waliiteketeza nyumba hiyo kwa moto.
|
No comments: