Mkazi wa Dar es Salaam, Goodluck Madaraka
anayedaiwa kujeruhiwa na risasi wakati wa mkesha wa sherehe ya harusi eneo la
Tabata Kisukulu usiku wa kuamkia jana, akiwa katika eneo hilo lililogeuka kuwa
la msiba jana, baada ya mwenzake Salim Ally kudaiwa kuuawa kwa risasi na jirani
yao aliyekerwa na kelele za muziki wakati wa sherehe hiyo.
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, mwanamume mmoja amewafyatulia risasi watu wawili na
kusababisha kifo cha mmoja kwa kile kinachodaiwa kumletea usumbufu wakati wa
mkesha wa harusi.
Mkuu
wa Upelelezi wa Mkoa wa Ilala, David Mnyambuga amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo ingawa hakuwa tayari kulizungumzia kwa madai kuwa siyo msemaji na
anayetakiwa kufanya hivyo ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala ambaye
hakupatikana kulizungumzia hilo.
Majeruhi
wa tukio hilo, Goodluck Madaraka aliyejeruhiwa na risasi zilipokuwa zinapigwa
hewani, alisema saa tano na nusu usiku walipokuwa wanacheza muziki kwenye
mkesha wa harusi, ghafla jirani yao aliyefahamika kwa jina la Lucas Muhabe
alikuja na panga na kuwafukuza kwa madai kuwa wanampigia kelele.
Alisema
Muhabe aliondoka na baada ya muda alirudi na bastola na kupiga risasi ovyo na
kwa bahati mbaya ikampata begani Mahamudu Muhasi aliyekuwa anapita njia na
kumpiga nyingine ya kichwa na kumuua papo hapo.
“Muhasi
alikuwa anapita njia hivyo hata vijana walivyokimbia yeye hakukimbia na
alipopigwa risasi ya bega la kushoto alilalama kumwambia huyo baba kuwa
anamwonea kwani hafahamu kitu chochote, cha kushangaza baada ya kuambiwa hivyo
aligeuka na kumpiga nyingine ya kichwa na kufariki dunia papo hapo,” alisema
Madaraka.
Madaraka
alisema kuwa kwenye heka heka za kupigwa risasi hizo moja ilimpitia kwenye
shavu na kumpasua na alikwenda Hospitali ya Amana na kushonwa nyuzi tatu.
Kaka
wa marehemu, Salim Ally alisema kuwa Muhasi alikuwa anashinda kwake na kulala
kwa mjomba wake mbali kidogo kutoka kwake, siku ya tukio baada ya kula chakula
cha usiku na kuzungumza hadi saa tano usiku, alimsindikiza.
Alisema
alipohakikisha wamepita kwenye maeneo ambayo hakuamini kama ni salama,
alimwacha aende mwenyewe, njia kuu ikiwa ni hapo palipokuwa na mkesha wa harusi
na alipata taarifa ndugu yake ameuawa kwa kupigwa risasi.
“Amekuja
mwezi wa saba kutoka Malinyi Ulanga, siyo mwenyeji na wala hashindi maeneo
hayo, ndiyo maana hata wakati vijana wanakimbia alikuwa anashangaa tu ndiyo
akapigwa risasi, inauma sana hata siamini kama sheria itachukua mkondo wake kwa
jinsi ninavyoumia,” alisema Ally.
Ally
aliongeza kuwa, tunasikia mtuhumiwa amesema marehemu ni jambazi ndiyo maana
amempiga risasi, kitu ambacho siyo kweli hana historia hiyo na ni mgeni hapa
jijini.
Akizungumza
na gazeti hili Mtawala Amani ambaye nyumbani kwake ndiyo kulikuwa na mkesha wa
harusi, alisema muda wa saa tatu aliamua kujipumzisha barazani aliamshwa mnamo
saa tano na nusu na kelele zilizokuwa zinatokea nje ya nyumba yake.
Alisema
baada ya kutoka nje alikuta damu na mwili wa kijana Muhasi na kuambiwa kuwa
jirani yao Lucas Muhabi ndiyo amemuua kwa kumpiga risasi na muda siyo mrefu
polisi walifika na kuuchukua mwili kuupeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mke wa Amani, Pili Miraji alisema kuwa anamfahamu marehemu kwa kuwa alikuwa akimwona anapita maeneo hayo na anakwenda kwa mjomba wake ambako siyo mbali kutoka hapo kwao.
Mke wa Amani, Pili Miraji alisema kuwa anamfahamu marehemu kwa kuwa alikuwa akimwona anapita maeneo hayo na anakwenda kwa mjomba wake ambako siyo mbali kutoka hapo kwao.
Mwisho
No comments: