Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Moshi Mjini, Zakaria Laizer amepewa likizo ya lazima ya siku 30, akituhumiwa kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Kiini cha kupewa likizo hiyo kinatokana na kukutwa akipata chakula na viongozi wawili wa zamani wa CCM katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, ambao sasa wamehamia Chadema.
Viongozi hao ni katibu wa zamani wa Itikadi na Uenezi wa mkoa wa Arusha, Issack Kapriano maarufu Kadogoo na Katibu wa zamani wa Uchumi na Fedha mkoa Kilimanjaro, Paul Matemu.
Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi, Loti Ole Nesele ametithibitishia jana kuwa Laizer kapewa likizo hadi baada ya uchaguzi.
“Miye sipo Moshi niko Babati, lakini ni kweli alipewa barua hiyo ya likizo wiki iliyopita, ukiniuliza sababu sitakwambia kwa sababu ni siri za mtumishi na ofisi,” alisema.
Hata hivyo, chanzo cha habari cha uhakika kinasema, Kadogoo ambaye ana undugu na Laizer alimpigia simu ndugu yake huyo akimjulisha kuwa angepita Moshi akienda Mwanga, hivyo amsaidie kumwekea oda ya chakula, naye akafanya hivyo katika mgahawa wa East African ambapo walikutwa na kiongozi mmoja wa CCM.
Mtu aliye karibu na Kadogoo, alisema katibu huyo alimpigia simu Matemu ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi ili ajumuike nao chakula cha jioni.
Taarifa hizo zinadai siku iliyofuata, Laizer aliitwa na kuhojiwa na viongozi wa CCM, lakini akajitetea kuwa Kadogoo ni mjomba wake na asingeweza kumtenga kwa vile amehamia Chadema.
Laizer ni miongoni mwa wana- CCM waliokuwa wakimuunga mkono Lowassa wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.
Kutokana na tuhuma za kuendelea kushirikiana na mgombea huyo wa Ukawa, viongozi hao walipendekeza kwa uongozi wa mkoa wa Jumuiya hiyo umpe likizo ya lazima Laizer kwa siku 30, ili arejee baada ya Uchaguzi Mkuu kumalizika.
Laizer alipoulizwa kuhusu likizo hiyo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo lakini mwenzake, Matemu licha ya kukiri kukaa meza moja na Laizer siku hiyo, alieleza kushangazwa na likizo akisema mjumuiko walioufanya haukuwa na ajenda yoyote ya kisiasa.
“Nimejiuliza maswali mengi lakini sipati majibu. Kwamba CCM imefika mahali inataka wana CCM wasichanganyikane na wafuasi wa vyama vingine. CCM wanataka kufanya siasa ni uadui?” alihoji.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM mkoa Kilimanjaro, Festo Kilawe, alipoulizwa kuhusu sakata hilo, aliomba aulizwe katibu wa jumuiya hiyo mkoa wa Kilimanjaro, Robert Chilamato.
Hata hivyo, Chilamato ambaye ndiye aliyesaini barua ya likizo hiyo, alitaka watafutwe viongozi wa wilaya wa jumuiya hiyo.
“Hilo jambo waulizwe viongozi wa wilaya (wa jumuiya) kwa vile mimi ni kiongozi wa ngazi ya mkoa,” alidai Chilamato. Chanzo MPEKUZI HURU
No comments: