Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, imeifuta hukumu iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ambaye alitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, kwa kosa la kumshambulia mwangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Nassir Uronu.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa Julai 17, mwaka huu, Mbowe alitozwa faini ya Sh. milioni moja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kupatikana na hatia.
Uamuzi wa kumfutia adhabu Mbowe, ulitolewa jana na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Aishiel Sumari, baada ya kusikiliza na kupitia hoja nne za rufaa namba 33/2015 iliyofunguliwa na Wakili Peter Kibatala.
Hata hivyo, wakati Mahakama Kuu ikimwondolea adhabu hiyo, Mbowe ambaye anagombea ubunge wa jimbo la Hai, hakuwapo mahakamani.
Jaji Sumari alisema Mahakama imesikiliza na kupitia kwa umakini hoja hiyo na kujiridhisha kwamba kulikuwapo na mkanganyiko wa shitaka na maelezo ya shitaka, hivyo kuathiri uhalali wa shitaka na uhalali wa hukumu iliyotolewa dhidi ya Mbowe.
“Katika msingi huo, Mahakama hii inaamuru Mbowe arejeshewe kiasi cha Shilingi milioni moja alizotozwa kama faini na Mahakama ya Wilaya ya Hai, katika kosa la jinai alilotiwa nalo hatiani, sababu za kuifuta hukumu hiyo zitatolewa mahakamani hapa Novemba 5, mwaka huu,” alisema Jaji Sumari.
Katika kesi ya msingi, Mbowe alishitakiwa kwa kosa la kumshambulia Uronu akiwa katika kituo cha kupigia kura cha Zahanati ya Machame Kaskazini, wilayani Hai.
Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tamari Mndeme, alidai kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali haipingani na rufaa hiyo kwa kuwa kuna utofauti katika shtaka na maelezo ya shtaka.
Katika rufaa hiyo, Mbowe alidai kuwa Mahakama ya Wilaya ya Hai ilimtia hatiani huku ikishindwa kushughulikia hoja muhimu katika kufikia uamuzi huo na kwamba ilishindwa kupima ushahidi kwa usahihi.
Pia alidai kuwa Mahakama ilishindwa kutilia maanani ushahidi wa mashahidi wa upande wa utetezi akiwamo yeye.
Aidha, alidai kuwa Mahakama hiyo ilishindwa kutumia msingi wa jukumu la kuthibitisha shtaka pale ilipoeleza kuwa mashahidi wa upande wa mashitaka walitoa ushahidi uliojitosheleza.
Kwa mujibu wa Mbowe, mahakama ilitakiwa kuutaka upande wa mashtaka uthibitishe shtaka bila ya kuacha mashaka, jambo ambalo alidai halikufanyika.
Kadhalika, Mbowe alidai kwamba Mahakama ilishindwa kueleza sababu zilizoifanya ishindwe kufikia uamuzi wake huo kama ilivyoelekezwa katika Sheria ya Mwendendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kufuatia sababu hizo, Mbowe aliiomba Mahakama Kuu iifute hukumu iliyomtia hatiani kuamuru arejeshewa Sh. milioni moja alizolipa kama faini.
No comments: