Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Murilo Jumanne Murilo akiagana na Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club - SPC) ,Kadama Malunde (kushoto) - Picha na Shinyanga Press Club.
*****
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Murilo Jumanne Murilo aliyekuwa kamanda Polisi Mkoa wa Shinyanga kuanzia Mwezi Agosti mwaka 2016 hadi mwezi Julai mwaka huu, leo Ijumaa Julai 21,2017 ameagana na Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga tayari kuanza kutekeleza majukumu yake ya Ukamanda wa polisi katika mkoa wa Kinondoni.
Julai 18,2017, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Saimon Sirro alifanya mabadiliko ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga.
Kufuatia mabadiliko hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Suzan Salome Kaganda amekuwa Mkuu wa kitengo cha Mafao na Fidia Makao Makuu ya Polisi na nafasi yake imechukuliwa na Kamanda Muliro huku nafasi ya Muliro ikichukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Sylverius Haule, ambaye alikuwa Afisa Mnadhimu wa Polisi wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza leo wakati wa kuagana na waandishi wa habari wa mkoa wa Shinyanga, Kamanda Muliro aliwashukuru wananchi wa mkoa wa Shinyanga pamoja na waandishi habari kwa ushirikiano waliokuwa wanampatia tangu afike mkoani humo.
“Mwezi Agosti mwaka 2016,nilipoteuliwa kuwa kamanda wa polili mkoa wa Shinyanga,kitu cha kwanza nilichokifanya nilikutana nanyi na kuwaomba ushirikiano wenu wa dhati katika utekelezaji wa majukumu yangu,nimeona niwashukuru kwa dhati,nawashukuru wadau wote wa masuala ya kiusalama katika mkoa wa Shinyanga,viongozi wa idara mbalimbali za serikali,wananchi pamoja na wanahabari ambao kwa kiwango kikubwa walinisaidia katika kutekeleza majukumu yangu”,alieleza Kamanda Muliro.
“Waandishi wa habari nawapa nafasi ya pekee kwa sababu tangu mwanzo niliwaeleza kuwa ili tuweze kutekeleza majukumu yetu ya masuala yanayohusiana na haki ninyi mna nafasi kubwa,niliwakumbusha kuwa ninyi mna nafasi ya kuona mbali wakati mwingine kuliko tunapoona sisi,mnapata habari mbalimbali ambazo zilikuwa zinatusaidia sana kufanya uchunguzi na kufanikisha kutoa haki kwa wananchi”,alisema Kamanda Muliro.
“Wote mnakumbuka changamoto tulizokuwa nazo mkoani hapa,ikiwemo za wazee kuuawa,unyang’anyi wa kutumia silaha,utekaji magari,ajali za barabarani,makosa ya ndoa za utotoni,watu kujichukulia sheria mkononi kwa kupitia ninyi mmenisaidia sana,tulipambana wote kwa pamoja na kwa kiasi kikubwa tukafanikiwa na kuufikisha mkoa hapa tulipofika”,alisema Kamanda Muliro.
“Nimewaiteni hapa ili kuwapa taarifa rasmi kuwa sasa naenda kutumikia mkoa wa Kinondoni,naomba kamanda anayekuja mmpatie ushirikiano mlionipa,muwe wawazi,watulivu,wavumilivu na jambo lolote mnaloona au kulisikia muweze kulifanyia uchunguzi na wakati mwingine mpate habari upande wa pili kama vile taaluma zenu zinavyoelekeza”,aliongeza Kamanda Muliro.
Akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga,Kadama Malunde alimshukuru kamanda Muliro kwa ushirikiano wote aliokuwa akitoa kwa waandishi wa habari kwa muda muafaka pale walipohitaji ufafanuzi kuhusu mambo mbalimbali ili kuihabarisha na kuielimisha jamii ili kufichua na kutokomeza vitendo vya kihalifu mkoani humo.
“Kamanda Muliro hakuwa na tabia ya kupuuzia mambo anayoelezwa,alikuwa msikivu siku zote amekuwa akitumia kauli ya “Jifunze Kusikiliza”,na mara kwa mara amekuwa akifika katika ofisi ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga siyo tu kikazi bali hata kubadilishana tu mawazo”,aliongeza Malunde.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Murilo Jumanne Murilo akizungumza na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Julai 21,2017 katika ukumbi wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club - SPC) ,Kadama Malunde akizungumza wakati Kamanda Muliro akiagana na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Murilo Jumanne Murilo akiagana na Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club - SPC) ,Kadama Malunde.
Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club - SPC) ,Shaaban Alley akifurahia jambo na Kamanda Muliro.
Wa kwanza kushoto ni Katibu Mtendaji wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga (SPC) , Stephen Wang'anyi,akifuatiwa na Mwenyekiti wa SPC,Kadama Malunde,kamanda Murilo na Makamu Mwenyekiti wa SPC ,Shaaban Alley wakiwa katika picha ya kumbukumbu.
Waandishi wa habari mjini Shinyanga wakiwa katika picha ya kumbukumbu na kamanda Muliro.
Waandishi wa habari waliopo mjini Shinyanga wakiwa katika picha ya pamoja na kamanda Muliro. Hawa ni miongoni mwa waandishi wa habari 91 waliopo mkoani Shinyanga ambapo kati yao zaidi ya 50 wapo mjini Kahama.
Baadhi ya Waandishi wa habari waliopo mjini Shinyanga wakiwa katika picha ya pamoja na kamanda Muliro.
Picha zote na Shinyanga Press Club
No comments: