Serikali imeeleza mikakati mbalimbali inayotekelezwa ili kuondoa changamoto za watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani, ikiwa ni pamoja na hatua za kinga, uokoaji na uimarishaji wa ustawi wa jamii katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Martha Festo Mariki, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kina yenye lengo la kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na kuepuka kuingia katika maisha ya mitaani.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa malezi bora na usimamizi wa watoto ili kuzuia hali zinazoweza kuwasukuma watoto kukimbilia mitaani.
Aidha, Serikali imeendelea kuhamasisha wazazi na walezi kutoa taarifa kwa maafisa ustawi wa jamii pale inapojitokeza changamoto zinazoweza kuhatarisha ustawi wa watoto ndani ya familia, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Katika kuimarisha usalama wa watoto, wazazi, walezi pamoja na walimu wanahimizwa kutoa taarifa mara moja katika vituo vya polisi au mamlaka husika pindi mtoto anapopotea nyumbani au shuleni, ili kusaidia ufuatiliaji wa haraka.
Serikali pia imeweka mkazo katika kuboresha uchumi wa kaya, hatua inayolenga kuhakikisha familia zinakuwa na uwezo wa kuwapatia watoto mahitaji yao ya msingi na hivyo kupunguza uwezekano wa watoto kuingia mitaani kutokana na changamoto za kiuchumi.
Vilevile, Serikali imeanzisha Madawati ya Huduma za Ustawi wa Jamii katika vituo vya usafirishaji nchini, yakiwa na jukumu la kubaini, kuzuia na kuwasaidia watoto wanaotoroka nyumbani na kuingia katika maisha ya mitaani.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, jumla ya watoto 6,182 waliokuwa wakiishi au kufanya kazi mtaani wameokolewa. Kati yao, watoto 5,663 wameunganishwa tena na familia zao, huku wengine waliobaki wakipatiwa huduma stahiki kulingana na mahitaji yao ya ustawi wa jamii.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha mikakati hiyo ili kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya kuishi katika mazingira salama, yenye malezi bora na yenye kumlinda dhidi ya changamoto za maisha ya mitaani.
Tags:
habari
