Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Dkt. Evaline Munisi, amewasisitiza waajiri sekta ya migodi kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu kima cha chini cha mshahara kilichowekwa na Serikali, akibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda haki za wafanyakazi na kuboresha ustawi mahali pa kazi.
Dkt. Munisi amesema hayo leo Julai 1, 2026 wakati wa ziara ya kikazi katika Mgodi wa Polygold uliopo Ikungi, Wilaya ya Musoma Vijijini, Mara iliyolenga kukagua utekelezaji wa Sheria za kazi.
Akizungumza na menejimenti ya mgodi huo pamoja na wafanyakazi, Dkt. Munisi amesema waajiri wa kimataifa wanapaswa kutoa kipaumbele kwa wazawa katika nafasi za ajira akieleza kuwa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kuona wananchi wakinufaika moja kwa moja na miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini.
“Mheshimiwa Rais anataka kuona tabasamu kwa waajiri na waajiriwa, hivyo ni wajibu wa kila mwajiri kuzingatia misingi, sheria na miongozo iliyowekwa na Serikali ili kujenga mazingira bora ya kazi na kudumisha mahusiano mazuri kazini,” alisema Dkt. Munisi.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ukaguzi, Bw. Emanuel Mwenda, amesema Serikali itaendelea kuimarisha ukaguzi katika maeneo ya kazi ili kuhakikisha waajiri wanazingatia sheria za kazi, mikataba ya ajira na viwango vya mishahara vilivyowekwa. Ameongeza kuwa Idara ya Kazi itaendelea kufanya kaguzi mara kwa mara ili kulinda haki za wafanyakazi, kuimarisha uzalishaji na kujenga mazingira bora ya kazi yanayowanufaisha waajiri na waajiriwa kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Naye, Mkurugenzi wa Mgodi wa Polygold, Bw. Milos banicévic, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa wawekezaji wa kimataifa, huku akiahidi kuwa mgodi huo utatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali ili kuhakikisha unaendana na kasi ya maendeleo.
Kwa upande mwengine, Bw. Julius Odhiambo, akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa mgodi huo, ameishukuru Serikali kwa kufika mgodini kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi, akisema hatua hiyo imeongeza imani yao kwa Serikali na kuonyesha dhamira yake ya kulinda maslahi ya wafanyakazi.
Ziara hiyo ya Naibu Waziri Munisi ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano katika kuhakikisha sheria za kazi, haki za wafanyakazi na mahusiano mema kazini vinaimarishwa, sambamba na kuhakikisha uwekezaji unaendelea kutoa manufaa kwa Watanzania kupitia ajira, ustawi wa wafanyakazi na kukuza maendeleo ya uchumi wa Taifa.


