Mbunge wa jimbo la kahama James Lembeli
Mbunge wa Kahama, James Lembeli amemtuhumu Katibu Mkuu wa zamani
wa CCM, Yusuph Makamba kwamba alikuwa nyuma ya mpango mahususi wa kumhujumu ili
akose ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Lembeli, mmoja wa wabunge walio mstari wa mbele katika vita
dhidi ya ufisadi, alisema mpango huo ulitekelezwa kwa kueneza taarifa za
kuanzisha jimbo la Ushetu ambalo alitakiwa agombee badala ya Kahama, lakini
baadaye msamaria mwema alimpa taarifa kwamba jimbo hilo ni halipo.
Lembeli katika mahojiano yake maalumu na gazeti hili mjini
Dodoma alisema alipewa taarifa hizo saa chache kabla ya muda wa mwisho wa
kurudisha fomu za kugombea ubunge na kwamba tukio hilo lilimfanya afute fomu
yake ya kugombea mara mbili.
“Ulikuwa ni uhuni na ufisadi wa hali ya juu kisiasa,” alisema
mwanahabari huyo wa zamani katika mahojiano hayo maalumu yaliyofanyika mjini
Dodoma mapema wiki iliyopita.
Alisema mara ya kwanza alijaza kwamba anagombea Jimbo la Kahama
lakini alifuta na kuandika jimbo la Ushetu baada ya kupewa taarifa za
kuanzishwa kwa jimbo hilo na baadaye alifuta Ushetu na kuandika tena Kahama
baada ya kugundua kuwa ulikuwa mchezo mchafu.
“Baada ya kuruka viunzi, viongozi waandamizi wa CCM wa
Shinyanga, akiwamo Mwenyekiti wa Mkoa, Hamisi Mgeja walisusa kunifanyia
kampeni,” aliongeza Lembeli ambaye aliibuka na ushindi wa asilimia 54.5 kati ya
kura zilizopigwa.
Alisema mpango huo wa kumhujumu ulianza mapema pale baadhi ya
viongozi walipokuwa wakieneza kwamba yeye (Lembeli) hatakiwi na kwamba ukweli
siyo kwamba alikuwa hatakiwi na wananchi bali baadhi ya viongozi.
Hata hivyo, Makamba alipoulizwa alisema ni uzushi kwa kuwa kazi
ya kugawa majimbo ni ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, CCM kazi yake ni kusimamisha
tu wagombea.
“Niacheni nipumzike niendelee kula pensheni yangu. Sasa niko
Bumbuli natoka kuswali na ninakwenda kula Iddi, niacheni nipumzike jamani, kama
kuna maswali zaidi aulizwe katibu mkuu wa sasa,” alisema Makamba.
Hata hivyo, Lembeni katika mahojiano hayo alisisitiza:
“Ninachodhani walikaa chini na mambo haya yalifanyika Dar es Salaam na mbaya
zaidi katika ofisi ya Makao Makuu ya CCM kwa sababu ndio walioleta taarifa.”
Kwa mujibu wa Lembeli, taarifa kwamba kuna jimbo jipya la Ushetu
ambako ndiko alikozaliwa, zilimfikia yeye na wagombea wenzake saa 9:30 wakati
mwisho wa kurudisha fomu ilikuwa saa 10:00 jioni.
“Wagombea wote tulikuwa tumesharejesha fomu ya kugombea Jimbo la
Kahama. Ilipoletwa hiyo taarifa, Katibu wa CCM wa wilaya ya Kahama akawapigia
simu wagombea wote kuwa anatuita ofisini,” alisema mtangazaji huyo wa zamani wa
Shirika la Utangazaji la Ujerumani, Deutche Welle na kuongeza:
“Tulipofika pale akatuambia kuna habari mpya kwamba kuna jimbo
jipya la Ushetu, kwa hiyo hapa yako majimbo mawili kuna Jimbo la Kahama na kuna
jimbo la Ushetu.”
Pia, mwandishi huyo wa zamani wa gazeti la Kiongozi alisema
katibu huyo aliwaambia kuwa maelekezo aliyopewa kutoka makao makuu ya CCM ni
kuwataka kila mmoja afanye uamuzi papo hapo kama anagombea Kahama au Ushetu.
Lembeli alidai baada ya kuelezwa hivyo, alihoji sana ili kupata
ukweli kama jimbo hilo jipya limetangazwa na CCM au NEC.
“Yule katibu akapiga simu kwa mzee (katibu mkuu wa CCM wa wakati
huo, Yusuf Makamba) akawa ameacha sauti tusikie. Akamwambia ‘mzee hapa wagombea
wanahoji maswali mengi’,” alisema Lembeli.
“Makamba akauliza nani huyo, akaambiwa ni Lembeli, akasema ‘huyo
kijana ni mkorofi sana, mbishi sana huyo, kama hataki aache’. Nikachukua fomu
nikafuta Kahama nikaandika Ushetu.”
Lembeli alisema mpango uliokuwapo ni kumfanya (yeye) achukue
fomu ya jimbo ambalo halipo na atakapokuja kushtuka, muda wa kurudisha fomu na
kampeni uwe umeshakwisha.
“Wakati ule mtandao wa simu ulikuwa haujasambaa kwenye jimbo
zima. Muda wa mimi kufanya mashauriano kule kijijini haukuwapo na Ushetu ni
eneo ambalo nilizaliwa,” alisema.
“Nafsi ikaniambia nikigombea huku mjini bila kuwa nimewaarifu
kule nitakuwa nimewavunjia heshima kwa hiyo nikaamua iwe Ushetu. Sasa
tukawaambia leteni fomu mpya tujaze wakasema ‘futa hapo kwenye Kahama andika
Ushetu’. Nikafuta nikaandika Ushetu.”
Lembeli (58) alidai baada tu ya kufanya uamuzi huo, Mgeja ambaye
wakati huo alikuwa Dar es Salaam kwenye ofisi ya makao makuu ya chama, akamtuma
mke wake kuja kuchukua fomu za Jimbo la Kahama.
Kwa mujibu wa Lembeli, siku iliyofuata walianza kampeni kwa
ajili ya kura za maoni ndani ya chama wakati huo wakiwa wanaamini kuna jimbo
jipya la Ushetu limetangazwa na Nec.
Aliyemwokoa
Lembeli alisema: “Namshukuru sana (mtangazaji wa TBC jina
tunalo). Yeye ndio aliniambia ‘Lembeli mbona nasikia sikia jambo, huko kuna
nini?”
Alisema baada ya kampeni nzito za siku nne na walipokuwa
wakiingia siku ya tano ya kampeni hizo ndani ya chama, akahisi kuwa kuna mchezo
mchafu unaendelea.
“Nilipiga simu Tume ya Uchaguzi kuulizia nikaambiwa unasemaje,
eti jimbo la Ushetu? Ushetu ndio mnyama gani. Mzee, nilipata tumbo la
kuharisha,” alisema Lembeli.
“Yaani nilipoulizwa tu Ushetu ni mnyama gani nilipata tumbo la
kuharisha nikajua tayari nimeshapoteza nafasi,” alisema Lembeli katika
mahojiano hayo.
“Siku ya tano ikaja simu kutoka CCM ya kutuita wale tuliokuwa
tunagombea Ushetu wakatuambia makao makuu walikuwa wameghafilika kulikuwa
hakuna jimbo linaitwa Ushetu.”
“Kwa hiyo nyie mlikuwa mnagombea Ushetu kama mnataka kuendelea
kugombea Jimbo la Kahama futeni hapo Ushetu weka Kahama. Nikafuta Ushetu
nikaweka Kahama na hapo hapo Mgeja akajitoa,” alisema.
“Mimi naamini kulikuwa na mchezo kwa sababu kulikuwa na haja
gani ofisi kuu ya chama kusema kitu ambacho hakipo? Hata baada ya kushinda kura
ya maoni, bado vita ilihamia Dodoma,” alisema.
Baada ya kutokea sakata hilo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa wakati
huo, Rajabu Kiravu alilazimika kutoa ufafanuzi kuwa Tume ya Uchaguzi haikuwa
imeanzisha jimbo jipya la Ushetu kama ilivyokuwa imetangazwa awali na Katibu wa
CCM wa Wilaya ya Kahama, Sospeter Nyigoti ambaye ndiye aliyewaambia wagombea kuwa
Ushetu ni jimbo jipya.
Jina lake kupitishwa
Alisema katika majina yaliyochukua muda mrefu kujadiliwa katika
vikao vya chama vya uamuzi ya wagombea mjini Dodoma, lilikuwa lake.
“Namshukuru sana Rais Jakaya Kikwete kwa sababu ndiye
aliyesimama kidete kutaka haki itendeke,” alisema Lembeli ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Lembeli alisema baada ya jina lake kupitishwa, viongozi wakubwa
ndani ya chama Mkoa wa Shinyanga hawakukanyaga kwenye Jimbo la Kahama kumfanyia
kampeni diwani, mbunge wala Rais.
“Viongozi waandamizi wa chama hawakugusa kabisa kwenye kampeni
kwenye jimbo langu. Kwa maana hiyo, mkoa haukumfanyia kampeni Rais kwenye jimbo
la Kahama,” alisema.
“Niliachwa peke yangu lakini walitaka kumuonyesha mwenyekiti
(Kikwete) siwezi ili kama nikishindwa, waseme ‘si unaona tulikwambia kwamba
huyu bwana hakubaliki’.”
Lembeli alisema pamoja na yeye kushinda kura ya maoni kwa
tofauti ya kura nne tu, lakini alipokwenda kwa wananchi aliibuka na ushindi wa
kishindo kwa kupata kura 32,531.
Wagombea wengine katika jimbo hilo walikuwa Dotto Lubala wa
Chadema aliyepata kura 20,912 na Hassan Makapa wa CUF aliyeambulia kura 3,950.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
No comments: