Mgombea
Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, jana
aligeuka mbogo baada ya kuamua kuwataja hadharani watu wanaohujumu
kampeni zake kwa kujifanya mchana wako pamoja na usiku wakigeukia upande
wa upinzani.
Akiwahutubia
wananchi wa mkoani Shinyanga jana katika mkutano wake wa kampeni
uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage, Dk. Magufuli, alisema kuna
mamluki wanaokihujumu chama hicho katika kuelekea uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Dk. Magufuli aliwataja hadharani baadhi ya makada hao ambao wamekuwa
wakiipigia kampeni CCM mchana na usiku wakiwapigia wapinzani.
“Kuna baadhi ya wana-CCM wanatujuhumu sana, wengine nawajua hata majina
yao bahati nzuri huwa sisemi uongo bali ukweli, kuna huyu Gasper mchana
tunakuwa naye CCM lakini usiku anaungana na wapinzani,” alisema.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Dk. Magufuli ilipokelewa kwa mshangao na
baadhi ya wananchi na wanachama waliokusanyika uwanjani hapo, kwa kuwa
baadhi ya makada hao walikuwa wameketi jukwaa kuu wakifuatilia hotuba
yake.
Waandishi wa habari hizi walimshuhudia meneja kampeni wa mgombea huyo,
Abdallah Bulembo, akimfuata Magufuli na kumnong’oneza ,ghafla Magufuli
alibadilisha na kudai msaliti ni Gasper Anthony wala si Gasper Kileo
aliyetajwa awali.
Hata hivyo, Magufuli baada ya kumaliza hotuba yake alimfuata kada wa
CCM mkoani Shinyanga anayetumia jina la Gasper aliyeonekana kupaniki na
kumkumbatia huku akimtuliza na kuendelea na msafara wake.
No comments: