HISTORIA YA MAREHEMU MCHUNGAJI MTIKILA, JINSI ALIVYOANZA SAFARI YA MAISHA YA SIASA TANZANIA
MCHUNGAJI Christopher Mtikila ni Mwenyekiti wa chama cha Democratic Party (DP) ambacho kina usajili wa kudumu hapa nchini.
Mtikila alizaliwa mwaka 1950 mkoani Iringa, kusini mwa nchi yetu.
(Kwa bahati mbaya, hadi nachapisha uchambuzi huu sikupata taarifa za
elimu yake) kwani hakuwa mwepesi kutoa ushirikiano mwezi mmoja uliopita
alisafiri kwenda nje ya nchi na kurejea wakati nikiwa katika hatua za
mwisho za uhariri.
Pamoja na shughuli za siasa, Mchungaji Mtikila ni mwanzilishi na mkuu wa
kanisa la Kipentekoste la Full Salvation Church. Lakini pia kwa muda
mkubwa wa maisha yake amekuwa anajihusisha sana na harakati za haki za
binadamu kwa kupitia kitengo cha haki za binadamu cha kanisa hilo
kiitwacho “Liberty Desk”.
Kanisa lake ni moja ya makanisa machache sana hapa Tanzania yenye vitengo vya namna hiyo.
Umaarufu wa Mtikila ulikua sana mwanzono mwa miaka ya 1990 kutokana na
uwezo wake mkubwa wa kuongea, upinzani wake dhidi ya muundo wa muungano
kati ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu kile anachokiita
“uhujumu wa uchumi unaofanywa na wahindi” (ambao anawaita Magabacholi),
na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika mahakama za
Tanzania,ni kati ya mambo machache yaliyofanya asikike kila kona ya
nchi.
Kwa muda mrefu chama chake cha DP hakikuweza kupata usajili wa kudumu
kutokana na kukataa kwake kuitambua Zanzibar, alikuwa akisisitiza kuwa
chama chake ni cha Tanganyika na sio Tanzania.
Hata hivyo Mtikila ilimpasa abadili msimamo wake katika miaka ya hivi
karibuni kwa kukubali kutafuta wanachama toka Zanzibar (kama sheria ya
uchaguzi inavyotaka) na hivyo chama chake kilipata usajili wa kudumu.
Mtikila alifungwa kwa mwaka mmoja mwaka 1999 baada ya kupatikana na
hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu wa CCM,
marehemu Horace Kolimba.
Mwaka 2004 pia alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa
kutoa maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala. Kwa
ujumla maisha yake yamekuwa ni ya harakati muda wote, akipambana
awezavyo, akisimama kidete inavyowekana na akijikuta matatani kila
uchwao. Mchungaji Mtikila amemuoa Bi. Georgia na wana watoto.
MBIO ZA UBUNGE
Mwaka 1997, Mbunge wa jimbo la Ludewa kwa tiketi ya CCM, Horace Kolimba
aliitwa na Kamati Kuu ya chama chake mjini Dodoma kwenda kujibu mashtaka
ya ndani ya chama juu ya kauli ambazo alikuwa akizitoa kwamba “CCM
imepoteza mwelekeo”, baadhi ya viongozi wa chama chake walimchukulia
kama msaliti na wengine wakimuona kama mtu aliyethubutu kusema ukweli
bila kumuhofia Nyerere.
Hata hivyo Kolimba alifariki hukohuko Dodoma katika siku ambazo alikuwa
akihojiwa. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipotangaza kukuwepo kwa uchaguzi
mdogo, ndipo Mchungaji Christopher Mtikila, alikihama chama chake cha DP
akajiunga CHADEMA na kuomba ridhaa ya kugombea jimbo la Ludewa, Chadema
ikampa ruhusa hiyo.
Mtikila ni mzaliwa wa Ludewa na alifanya hivyo kwa sababu chama chake cha DP kilikuwa kimenyimwa usajili.
Uchaguzi wa Marudio ulifanyika tarehe 25 Mei 1997 na kumpa ushindi
mgombea wa CCM Prof. Chrispin Haule Che Mponda. Prof Mponda alipata kura
20,111 dhidi ya kura 8,386 za Mchungaji Christopher Mtikila wa CHADEMA.
Mgombea wa NCCR ambayo haikuwa imejijenga vilivyo Ludewa, Barnabas
Kidulile, alipata kura 1,271.
Hata hivyo, baada ya kushindwa uchaguzi huo, Mchungaji Mtikila alisikika
akihitilafiana na CHADEMA hadharani huku akiipa shutuma nzito nzito,
akafukuzwa kwenye chama hicho na ndipo akaendelea kuwekeza nguvu kwenye
mipango ya kukamilisha usajili wa chama chake.
MBIO ZA URAIS
Mtikila alianza rasmi harakati za kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania mwaka 2005 kwa tiketi ya DP alikuwa kati ya wagombea 10 wa
nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.
Katika uchaguzi huo alipata kura asilimia 0.27 ya kura zote, akiwa nyuma
ya Jakaya Kikwete wa CCM (asilimia 80.28), Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF
(asilimia 11.68), Freeman Mbowe wa CHADEMA (asilimia 5.88), Augustine
Mrema wa TLP (asilimia 0.75) na Dkt. Sengondo Mvungi wa NCCR (asilimia
0.49).
Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Mtikila hakugombea nafasi ya Urais na
chama chake hakikuweka mgombea na kwa mwaka huu 2015 hajaweka msimamo
wake wazi japokuwa taarifa za ndani ya chama hicho zinaonesha kuwa
kinaweza kusimamisha mgombea na mtu huyo akawa ni Mtikila.
Nimemuweka katika Orodha hii kwa sababu tayari anatajwa kuwa na
sifa,vigezo na hata historia ya mapambano inayompa nafasi ya kuweza
kusimama mbele ya watanzania kuomba uongozi wa juu.
NGUVU YAKE
Jambo la kwanza ambalo bila shaka linampa Mtikila nguvu ikiwa ataingia
kwenye kinyang’anyiro cha urais ni umaarufu wake. Mtikila ni maarufu
sana, si kwa watu wenye umri wa zamani tu, lakini pia hata kwa vijana
wadogo wa sasa.
Ni vigumu sana kama mtanzania yeyote anafuatilia masuala ya siasa katika
nchi au anafuatilia habari mara kwa mara na asimjue Mtikila. Ni
kiongozi anayejishughulisha na mambo mengi mno na harakati
zilizopitiliza na kwa mwanasiasa anayetaka nafasi ya juu, umaarufu
unaweza kuwa karata muhimu, la msingi tu umaarufu huo vichwani mwa watu
uwe na maana ya kumuona kama “mtu muhimu” katika hatua zake.
Lakini jambo la pili linalompa nguvu na sifa zaidi, ni kazi kubwa ambayo
amekuwa akiifanya mara kwa mara, ya kufungua kesi za masuala ambayo
serikali inakuwa imewanyima raia kwa muda mrefu. Mara nyingi katika
siasa za Afrika, kesi za kuishtaki serikali kwa masula ambayo
yanaonekana kuwa makubwa huwa linaonekana kama jambo hatari hata kwa
usalama wa mhusika, Mtikila.
Kesi za kikatiba ambazo amewahi kufungua ni pamoja kesi ya kutaka
wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania, wananchi wa
Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasipoti, na vyama vya
siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba kibali toka kwa Mkuu wa
Wilaya na polisi n.k. Hebu tujiulize, ni vyama vingapi vya siasa
vimewahi kuwa na “uthubutu” huo?
Mtikila alishinda kesi ya mgombea binafsi na aliiweka serikalini kwenye
njia panda kwa asilimia mia moja. Katika suala hili yeye ni mtu wa
kujivunia sana na kama upiganaji wa kiwango hiki peke yake ndiyo
ungekuwa tiketi ya urais basi Mtikila tayari angestahili tuzo hiyo bila
mjadala. Hakuna mwanasiasa mwingine yeyote hapa Tanzania aliyewahi
kupambana na serikali mahakamani kila kukicha kama Mtikila, hayupo!
Lakini jambo la tatu linalompa nguvu na sifa ni ni Misimamo ya kipekee.
Mtikila hajali anapokuwa ana ajenda zake na misimamo yake na mara nyingi
misimamo hiyo huwa ni ya kipekee hata kama ni mibaya kiasi gani, yeye
huisimamia na kubakia nayo hata kama wenzake wote mtamkimbia.
Nakumbuka tulipokuwa Bunge Maalum la Katiba, Mtikila alikuwa na ajenda
ya kusimamisha bunge lile lisifanye kazi kwa sababu limeanza kinyume na
sheria na halina hadi ya kutunga katiba ya nchi. Pamoja na wanasheria
wakongwe sana kuwa na mawazo tofauti naye, bado alishikilia msimamo wake
na aliondoka kwenda Dar Es Salaam kwa minajili ya kufungua kesi husika
(sina taarifa jambo hili lilipoishia).
Na hata baadaye, vyama vinavyounda UKAWA vilipoamua kutonoka Bungeni,
Mtikila aliunga mkono uamuzi huo na alisisitiza kuwa yeye anafanya kazi
na umoja huo kwa suala la katiba, sijapata taarifa za hatma yake katika
kuendelea kuwa ndani ya UKAWA, lakini nachojua ni kwamba misimamo hii ya
Mtikila kuna wakati imekuwa na tija kubwa sana, si kwake tu bali kwa
taifa zima.
UDHAIFU WAKE
Udhaifu wa kwanza wa Mtikila ni utoaji wa “Kauli tata” ambazo kuna
nyakati zinaudhi na kuamsha hasira ya upande uliotuhumiwa. Mtikila ana
tabia ya kuongea mambo magumu na mkishindana sana akakudharau huweza
kukuita jina baya sana ambalo hukuwahi kufikiri kuwa unaweza kuitwa au
kupewa.
Mara kadhaa amewahi kusikika akitoa shutuma kali sana kwa viongozi wa
nchi, vyama vya upinzani n.k. Sifa hii ya Mtikila si sifa sahihi sana
kwa mtu ambaye ana ndoto au anaotewa ndoto za kushika uongozi wa juu
wanchi siku moja.
Lakini jambo la pili ambalo naliona kama udhaifu pia, Mtikila hupenda
kushughulikia mambo ya hatari peke yake na wakati mwingine bila kufanya
kazi ya kutosha kuwaelimisha wananchi na vyombo vya habari na kutafuta
hali ya kupewa uzito na mioyo ya wananchi na wadau.
Tabia hii ya Mtikila ya kuamka na ajenda nzito mkononi na kulazimisha
ajenda anayotoa iungwe mkono ghafla bila kuwaandaa wananchi, siyo jambo
zuri kisiasa.
Kuna masuala ya msingi sana anayapigania na yanapotoshwa na vyombo vya
habari, na wanasiasa wa vyama vingine n.k kwa sababu tu hakufanya kazi
ya siasa ya kuyatangaza masuala hayo, kuomba ushirikiano wa wenzake n.k.
Ili uwe kiongozi mzuri una wajibu wa kuwashirikisha watu waliokuzunguka
maamuzi makubwa unayotaka kuyafanya ili uungwe mkono. Kujifanyia peke
yako kunakuwa hakuna tija kubwa kwa maslahi mapana ya wote.
Na mwisho, Mtikila amekuwa akitoa kauli zinazodhaniwa kuwa ni za
kibaguzi sana na hili haliko “uvunguni”, amefanya hivyo mara nyingi mno
katika mikutano yake na hata mbele ya vyombo vya habari.
Kuna wakati amekuwa akisikika hadharani akiwatuhumu Wahindi kwa lugha za
kibaguzi sana, anawaita “Magabacholi”, lakini pia kuna wakati amewahi
kulalamikiwa hata na nchi jirani ya Rwanda kwa namna alivyowahi
kuyashutumu makabila makubwa ya nchi hiyo kwa kauli za kibaguzi.
Kiongozi mmoja wa juu wa Serikali nimewahi kumsikia akisema kuwa
alipokutana na Rais Kagame wa Rwanda, baada ya salamu Kagame akamuuliza
kiongozi huyo “Who is Reverend Mtikila”? (Mchungaji Mtikila ni nani?).
Mtikila siyo tu kuwa alikua anaipa chemsha bongo Serikali hapa ndani,
hata huko nje ya nchi wanaumiza vichwa juu yake na hili siyo suala la
kujivunia sana kama kweli nchi inatafuta viongozi watakaoimarisha
uhusiano na nchi za jirani.
No comments: