sponsor

sponsor

Slider

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

Kimataifa Habari

habari

Habari Za Mastaa

Michezo

simulizi za kusisimua

» » » Rais Magufuli aunga mkono uamuzi wa TCU kuvifungia vyuo 19

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewasili Jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Julai, 2017 akitokea Mkoani Dodoma ambapo akiwa katika eneo la Tegeta Wilaya ya Kinondoni amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na kero na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.


“Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa Tegeta, nianze kwa kuwashukuru sana, kwa kura nyingi mlizonipa ili niwe Rais wa Awamu ya Tano, nawashukuru CCM, nawashukuru CHADEMA, nawashukuru CUF, nawashukuru ACT na hata wale ambao hawana chama kwani wote kwa umoja wenu mlitanguliza maslahi ya Taifa na kumpa kura mtu ambaye atalisaidia Taifa, na mimi nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote na kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu ili Watanzania wote hasa wanyonge ambao siku zote walikuwa wakionewa” amesema Mhe. Rais Magufuli

Baadhi ya juhudi alizozitaja kufanyika tangu aingie madarakani ni pamoja na kuondoa ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Shilingi Bilioni 371 hadi kufikia Shilingi Bilioni 483, kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi na kulinda mali za umma hasa madini.

“Kwenye madini tumeibiwa sana, nchi yetu ni kati ya nchi zinazoongoza kwa kuibiwa, tumeibiwa kwa miaka 18, sasa imetosha” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuzuia udahili wa wanafunzi wote wa mwaka kwanza katika vyuo vikuu 19 na kuzuia udahili wa wanafunzi wa kozi 75 katika vyuo vikuu 22 kutokana na dosari zilizobainika wakati wa ukaguzi wa ubora vyuo hivyo uliofanyika Oktoba 2016.

“Ndugu zangu nchi hii ilishakuwa kila kitu hewa hewa, tumegundua wafanyakazi hewa zaidi ya 19,500, kulikuwa na mikopo hewa ya wanafunzi, na naipongeza TCU kwa kufungia baadhi ya vyuo kudahili wanafunzi, nafanya yote haya kwa ajili yenu, nataka tuwe na nchi nzuri”amebainisha Mhe. Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Julai, 2017

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply