NIMERIDHISHWA NA UTEKELEZAJI MAELEKEZO YA KUKAMILISHA JENGO LA OFISI YA MKUU WA MKOA MOROGORO NILIYOYATOA JANUARI 2026 - PROF. SHEMDOE

 


Na OWM – TAMISEMI, Morogoro 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema ameridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa maelekezo yake ya Januari, 2026 ya kutaka kukamilishwa kwa ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro ifikapo Julai 26, 2026. 

Prof. Shemdoe amesema hayo Juni 29, 2026 mjini Morogoro, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo ambayo ni sehemu ya muendelezo ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa ya ukamilishaji wa miradi ya mbalimbali ya maendeleo, yakiwepo ya utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. 

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa nimepata faraja kuona maendeleo ya ujenzi wa jengo hili lilofikia asilimia 90, Mhe. Mkuu wa Mkoa nikupongeze kwa ufuatiliaji na RAS kwa usimamizi wako mzuri,” ameeleza Prof. Shemdoe.

Kutokana na hatua nzuri ya ujenzi iliyofikiwa, Prof. Shemdoe amemtaka Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Musa, kuhakikisha watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wanahamia katika jengo jipya la ofisi hiyo ndani ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/27. 

Aidha, Prof. Shemdoe amemsisitiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Musa kuhakikisha lifti inaletwa na kuwekwa kwa wakati, ikiwa ni pamoja na kufanya maandalizi ya kupata samani mpya zitakazotumiwa na watumishi wa ofisi hiyo. 

Kufuatia uwekezaji uliofanywa, Prof. Shemdoe amesema kwamba jengo hilo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa likikamilika, litakuwa limetumia bilioni 6.5 hivyo amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo mkubwa aliofanya kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa mkoa wa Morogoro.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema atasimamia utekelezaji wa maelekezo ya Prof. Shemdoe na kufafanua kuwa maelekezo hayo yanapaswa kutekelezwa na ofisi yake kabla ya tarehe 30 Septemba 2026 saa sita usiku na si ifikapo Septemba 30, 2026.

Jengo hilo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro linajengwa na Mkandarasi MCB Company LTD, Mbeya University of Science and Technology kwa usimamizi wa Mshauri Elekezi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Post a Comment

Previous Post Next Post