PPAA YAWEKA MFUMO WA KIDIJITALI WA KUPOKEA RUFAA NA MALALAMIKO YA ZABUNI KUPITIA NEST

 Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), imeboresha utoaji wa huduma zake kwa kuanzisha moduli maalumu ndani ya Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Kielektroniki (NeST) inayowawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko na rufaa za zabuni popote walipo nchini.

Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma katika banda la PPAA, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando, alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa serikali wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema PPAA imeamua kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia kwa kuwa haiwezi kujitenga na mageuzi ya kidijitali yanayoendelea nchini, huku serikali ikiweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha huduma za umma zinapatikana kwa urahisi, haraka na kwa ufanisi zaidi.

“Tunachokifanya ni kutekeleza maelekezo tuliyoyapokea kutoka serikalini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye ufanisi mkubwa. Mfumo huu pia utatusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika usimamizi wa rufaa na malalamiko ya zabuni,” amesema Sando.

Amefafanua kuwa moduli hiyo ilianza kutumika rasmi mwezi Februari mwaka 2025 baada ya kuzinduliwa na Waziri wa Fedha wa wakati huo, ambaye amesisitiza matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za umma ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na urahisi wa upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Sando, matumizi ya mfumo huo yamepunguza utegemezi wa taratibu za ana kwa ana, hivyo kuwapa wananchi na wadau wa sekta ya ununuzi wa umma fursa ya kuwasilisha malalamiko na rufaa zao kwa njia ya mtandao bila kulazimika kusafiri hadi katika ofisi za PPAA.

Amesema PPAA itaendelea kuboresha huduma zake za kidijitali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi, huku taasisi hiyo ikipata uwezo mkubwa wa kushughulikia na kutatua migogoro ya zabuni kwa wakati na kwa ufanisi.

“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, za haraka na zenye uwazi, sambamba na kuimarisha utatuzi wa changamoto zinazohusiana na rufaa na malalamiko ya zabuni za umma,” amesisitiza Sando.

Post a Comment

Previous Post Next Post