
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Abwao, amefariki dunia leo Jumamosi, Juni 20, 2026, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, ambako alikuwa akiendelea na matibabu.
Kifo hicho kimethibitishwa na Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake, DCP David Misime, ambaye amesema SACP Abwao amefariki dunia leo baada ya kuugua na kuwa chini ya uangalizi wa madaktari katika hospitali hiyo.
"Ni kweli aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Richard Abwao, amefariki dunia leo tarehe 20 Juni 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu," amesema DCP Misime.
Ameongeza kuwa taarifa zaidi kuhusu chanzo cha ugonjwa wake pamoja na ratiba za mazishi zitatolewa na familia pamoja na mamlaka husika.
Akizungumzia msiba huo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amesema kifo cha SACP Richard Abwao ni pigo kubwa kwa Jeshi la Polisi na wananchi wa Mkoa wa Tabora kutokana na mchango wake mkubwa katika kuimarisha usalama, amani na utulivu wa mkoa huo.
Mhe. Chacha amesema marehemu alikuwa kiongozi aliyetekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na kujituma, hali iliyomjengea heshima kubwa ndani na nje ya Jeshi la Polisi.
Kifo cha SACP Richard Abwao kimeacha simanzi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, viongozi wa serikali, askari wa Jeshi la Polisi pamoja na wananchi wengi waliopata fursa ya kufanya kazi naye katika kipindi cha utumishi wake.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.
Tags:
habari