Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando amewaaga
wafanyakazi wa kampuni hiyo baada ya kumaliza mkataba wake wa miaka miwili na
nusu.
Mkataba wa Tido katika kampuni ya Mwananchi
utafika kikomo mwishoni mwa mwezi huu.
Taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Nation Media
Group (NMG), Linus Gitahi kwa wafanyakazi wote wa Afrika Mashariki ambako
kampuni hiyo inamiliki vyombo vya habari, inasema Mhando anaondoka MCL huku
akiacha mafanikio makubwa katika nyanja zote na kwamba atakumbukwa kwa mchango
wake.
MCL ni kampuni tanzu ya NMG inayochapicha
magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumamosi, Mwananchi Jumapili, The Citizen, The
Citizen on Saturday, Sunday Citizen na Mwanaspoti.
Kabla ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MCL mwaka
2012, Mhando alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC) kati ya mwaka 2006 na 2010. Awali alikuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili ya
Shirika la Utangazaji la BBC (1999-2006).
Mhando aliiwezesha MCL kukua kwa kasi kubwa
katika mapato na katika mpango wa uchapishaji wa magazeti ya MCL Kanda ya Ziwa
ambako wakazi wa mikoa hiyo sasa wamekuwa wakisoma magazeti asubuhi tofauti na
zamani
Wafanyakazi wa MCL walimpongeza kwa kuboresha
masilahi yao kwa kipindi cha uongozi wake na kuandaa misingi bora ya uongozi,
ikiwamo kumwandaa mrithi wake.
Akiwaaga wafanyakazi jana asubuhi, Mhando
aliwashukuru kwa ushirikiano wao pia alisema amejifunza mambo mengi mapya,
ikizingatiwa kuwa kwa miaka mingi alikuwa kwenye sekta ya habari ya utangazaji
tofauti na uchapishaji.
“Safari hii ilinipa uzoefu mpya na wenye changamoto
nyingi lakini kupitia ushirikiano wenu wa dhati tulifanikiwa kuiweka kampuni
katika hali nzuri,” alisema Mhando.
Gitahi alisema nafasi ya Mhando itachukuliwa
na aliyekuwa Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa MCL (COO), Francis Nanai.
Nanai alijiunga MCL , Agosti mwaka jana
akitokea Kampuni ya Saruji ya Mbeya Cement (Lafarge Tanzania) ya mkoani Mbeya
akiwa Mkurugenzi wa Biashara.
CHANZO: MWANANCHI
No comments: