Mwenyekiti wa ccm mkoa wa shinyanga khamis mgeja
Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja(pichani)
amesema kitendo cha Umoja wa katiba ya Wananchi (UKAWA) kutangaza kusimamisha
mgombea mmoja kuanzia ngazi ya mitaa hadi uchaguzi mkuu ili kuiangusha
CCM ni ndoto za mchana na kwamba hiyo ni dalili za kufirisika kisera na
kuchanganya wananchi.
Mgeja
aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa harambee kwa ajili
ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha Afya kata ya Kambarage
manispaa ya Shinyanga ambapo mgeni rasmi alikuwa naibu waziri wa nishati na
madini Stephen Masele ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini kupitia
CCM.
Alisema
kitendo cha vyama vya siasa vya upinzani nchini kuungana kusimamisha mgombea
mmoja ili kuiangusha CCM ni dalili za vyama hivyo kupoteza mwelekeo wa ki sera
na kuwachanganya wananchi washindwe kuelewa ni ilani au sera ipi itakuja
kutekelezwa na vyama hivyo.
“Hii
ni dalili ya watu hawa kufirisika ki sera,tunaweza kusema kuwa arobaini yao ni
safari hii kwamba sasa wametoka kwenye biashara ya jumla sasa wanaelekea
kufanya biashara ya reja reja,wananchi watashindwa kuelewa kwamba wanafuata
sera ya chama kipi,ili watakapokosea wananchi wawasute”,alisema Mgeja.
“Mimi
nafikiria mwisho wao umeshafika,wanatudhihirishia kuwa
wameishiwa,wamefirisika ndiyo maana wameamua wakusanye nguvu kuliangusha gogo
kitu ambacho hakitawezekana,Kwa kweli sasa Chadema,Cuf,NCCR Mageuzi Kushnei!!
Kwisha kabisa!!”,aliongeza Mgeja.
Alisema
CCM imefanya mambo makubwa chini ya rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwaletea
maendeleo wananchi katika sekta mbalimbali badala ya wapinzani ambao wao ajenda
yao ni matusi na kubeza mafanikio yaliyofikiwa na CCM.
“Tunahitaji
kuzungumza maendeleo,tusigeuze Shinyanga kama kituo cha watu kuja
kutukana,atakuja hapa Freeman Mbowe,atakuja Dr Wilbroad Slaa,atakuja Tundu Lisu
na matusi yao,hawaleti hata mfuko mmoja wa saruji,lakini Wanashinyanga
tutakesha tunashabikia oooh! Unaona bwana hili jembe,sisi hata majembe ya
matusi yanapongezwa”,alisema Mgeja.
Katika
hatua nyingine alimpongeza diwani wa kata ya Kambarage kupitia Chadema Nyangaki
Shilungushela kwa kuendesha siasa za kistaarabu bila matusi huku akiwataka
viongozi wengine wa Chadema kuiga mfano wake kwani kinachotakiwa ni ushirikiano
kuwaletea maendeleo wananchi.
“Kituo
hiki cha afya kiko katika kata inayoongozwa na Chadema,lakini ndugu yangu
Shilungushela siasa zake za kistaarabu sana,angekuwa mwingine matusi
yangetawala,lakini kakubali kushirikiana na mbunge kuwaletea maendeleo
wananchi,kwani kituo hiki kinatumiwa na watu wote bila kujali huyu ni wa
CCM,CUF au Chadema”,alieleza Mgeja.
Katika
harambee ya kuchangia ujenzi wa wodi ya wazazi kituo cha afya cha Kambarage CCM
mkoa wa Shinyanga walichangia mifuko 20 ya saruji,huku mbunge wa jimbo la
Shinyanga mjini Stephen Masele na rafiki zake wakichangia shilingi milioni 45.
Wadau
mbalimbali wajitokeza wakiongozwa na mbunge Masele aliyekuwa mgeni rasmi katika
changizo hilo na kufanikiwa kukusanya shilingi milioni 115 ikiwa ni zaidi ya
asilimia 100 ya pesa zilizokuwa zinahitajika shilingi milioni 105.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
No comments: