MKUU WA
MAJESHI YA ULINZI NCHINI (CDF) JENERALI DAVIS MWAMUNYANGE.
Watu 12 wamejeruhiwa
wakati wa mashambulizi ya kurushiana risasi baina ya askari wa Jeshi la
Wananchi (JWTZ) Kikosi 128 KJ cha Nyandoto na Polisi wa Kituo cha Stendi
wilayani Tarime mkoani Mara.
Hatua hiyo imekuja
wakati wanajeshi hao walipokuwa wakijaribu kumchukua askari mwenzao
aliyekamatwa na Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuendesha pikipiki
bila kuwa na kofia ngumu.
Mashambulizi hayo ya
kurushiana risasi na kutwangana ngumi na mateke yalitokea juzi saa 12 jioni
katika Kituo cha Polisi Stendi.
Mganga Mfawidhi wa
Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Bernard Makonyo alisema amepokea
majeruhi 10, kati ya hao wawili ni askari wa JWTZ, polisi saba na raia mmoja.
Alisema majeruhi tisa wameruhusiwa na mwingine kupelekwa Hospitali ya Shirati
kwa matibabu zaidi.
Dk Makonyo aliwataja
waliojeruhiwa kuwa ni Aloyce Filbert (24) aliyepigwa risasi mguu wa kulia,
Deodatus Dominic (26) aliyejeruhiwa puani na wote ni askari wa JWTZ.
Wengine ni askari
polisi saba ambao ni Makoye Katula (26), Sylvester Michael (31), Salum Omary
(44), Abdallah Halifa (24), Joel Msabila (25), Ally Juma (27) na Deogratius
Tryphon (32) na raia Hamza Jumanne (33) aliyepigwa risasi mguu wa kushoto
ambaye alipelekwa Hospitali ya Shitari, Rorya kwa matibabu.
Mkuu wa Upelelezi wa
Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Ndalama Salumu anadaiwa kujeruhiwa kwa kupigwa
katika vurumai hizo huku mwananchi mwingine, David Kisaro (20) akijeruhiwa kwa
bomu jichoni. Alitibiwa katika Zahanati ya Tarime.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kipolisi Tarime/Rorya, Benedict Mambosasa alisema mwanajeshi aliyekamatwa
alifanya makosa kwani baada ya kukamatwa na kuombwa kwenda kituo cha polisi,
alikaidi.
Mambosasa alisema
mwanajeshi huyo licha ya kukiuka taratibu, aliwatolea lugha za matusi polisi
jambo lililowalazimu kumkamata kwa nguvu, ndipo wanajeshi wenzake walipoingilia
kati na kusababisha kutokea kwa majibishano ya risasi za moto. Hata hivyo,
alisema hakuna aliyejeruhiwa.
Alisema wanajeshi
watatu ambao hawakutajwa majina, wamekamatwa na polisi kwa kuvunja utaratibu wa
usalama.
Mkuu wa Wilaya ya
Tarime, John Henjewele ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya Wilaya, amelaani kitendo hicho cha kurushiana risasi za moto hewani akisema
ni cha utovu wa nidhamu na maadili ya kazi ya jeshi na kwamba hatua kali
zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema wananchi
Tarime wameshangazwa kwa kitendo kilichofanywa na walinda usalama hao, wakisema
si cha kinidhamu huku wakisema kilikwamisha shughuli zao kwa muda kwa kuhofia
usalama wa maisha yao.
MWISHO
No comments: