Waziri
Mkuu Mizengo Pinda (mwenye tai) akisisitiza jambo mara baada ya kutembelea
maabara ya kisasa ya sayansi ya Chuo Kikuu cha Mkwawa (MUCE) Iringa, katika
ziara yake ya siku tano ya kutembelea miradi ya maendeleo mkoani Iringa.
AKIWA
katika siku ya tatu ya ziara yake ya siku tano mkoani Iringa, Waziri Mkuu
Mizengo Pinda amewaonya viongozi na chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM)
kuacha kuwachaguliwa wananchi viongozi.
Aliyasema
hayo kwa nyakati tofauti juzi, katika ziara aliyofanya katika vijiji vya Mlowa,
Magozi na Kiwele, wilayani Iringa, kutembelea shughuli za maendeleo.
“Mwaka
huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Hili ni zoezi muhimu sana kwa nchi ya
kidemokrasia kama hii. Tuwaache wana CCM na wananchi waamue wenyewe,
wasisirutishwe kuchagua viongozi wasiowataka,” alisema.
Alisema
wagombea hao ni kwa nafasi zote zitakazoshindaniwa katika uchaguzi huo ikiwemo
ya udiwani, ubunge na rais.
Alisema
CCM ikifanya makosa ya kuwapatia wananchi wagombea wasiowataka itaruhusu
wagombea wazuri kukimbilia upinzani na kujiweka katika hatari ya kuangushwa
katika uchaguzi huo.
“Tuwaunge
mkono wagombea wanaokubalika, wenye sifa ya kutuletea maendeleo. Tukifanya
makosa tutaanguka asubuhi tena anguko la mweleka,” alisema.
Alisema
pamoja na kuwapa wana CCM uhuru wa kuchagua, watajiangusha kama watawachagua
kwasababu ya rushwa au ofa mbalimbali zikiwemo bia.
Akizungumzia
umuhimu wa uchaguzi huo kwa CCM, Pinda aliwataka watanzania kwa ujumla wao kujiandikisha
katika daftarai la wapiga kura ili wawe na uhalali wa kuchagua viongozi
wanaowataka wakati ukifika.
“Tupo
katika hatua za mwisho za kuanza uandikishaji kwa kutumia teknolojia mpya ya
BVR na mimi mwenye nitafanya uzinduzi wa zoezi hilo mkoani Njombe,” alisema.
Waziri
Mkuu alisisitiza kila mwenye umri wa kupiga kura (kuanzia miaka 18 na
kuendelea) asiipuuze nafasi hiyo kwani mbali na kadi ya mpiga kura kupiga kura
lakini pia itatumika kama kitambulisho wakati mchakato wa kutoa vitambulisho vya
utaifa ukiendelea.
Kuhusu
Katiba Mpya, Waziri Mkuu aliwataka watanzania kutumia uhuru wao kujitokeza kwa
wingi kupigia kura ya ndio au hapana katiba hiyo inayopendekezwa.
“Jitokezeni
kwa wingi mkaipigie kura. Kazi iliyofanywa na bunge maalumu la katiba ilifanywa
kwa umakini mkubwa, ni katiba inayojali makundi yote katika jamii,
msiwasikilize wanaotaka msusie,” alisema.
Alisema
kabla ya zoezi hilo serikali itakahakikisha inasambaza nakala ya katiba hiyo
ili watanzania popote walipo waweze kuipitia ili wajiridhishe juu ya maeneo
yanayopotoshwa.
“Kwahiyo
tutsambaza katika kata zote, vijiji, mitaa, makundi ya kijamii na taasisi
mbalimbali zikiwemo za dini,” alisema.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu ameipongeza CCM Mkoa wa Iringa kwa kuongoza kitaifa katika
Uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba mwaka jana.
“Kwa
CCM, mkoa wa Iringa umeongoza kitaifa kwa kujipatia ushindi wa asilimia 98. Ni
asilimia mbili tu ndio tuliwaachia wapinzani na sehemu yake zimeto pale mjini
Iringa na tunajua ni kwasababu gani,” alisema.
Alisema
ushindi huo ni kiashiria tosha kwamba katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge
na Rais mkoa wa Iringa utafanya vizuri kama ilivyofanya katika uchaguzi huo wa
serikali za mitaa.
Mwisho
No comments: