Naibu Waziri
wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Tate Ole Nasha (MB) (mwenye
tai) akikaribishwa katika Banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya
Tanzania (TADB) mara baada ya kufungua Maadhimisho ya Kampeni ya Wiki ya
Maziwa inayofanyika Kitaifa mjini Bukoba, mkoani Kagera kuanzia tarehe
28 Mei had Juni 01.
Afisa Mahusiano na Masoko Mkuu wa TADB,
Bw. Saidi Mkabakuli (kushoto) akizungumza wakati Naibu Waziri wa Kilimo
Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Tate Ole Nasha (MB) (mwenye tai)
alipotembelea Banda la TADB.
Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi
Mheshimiwa William Tate Ole Nasha (MB) (mwenye tai) akizungumza na
maafisa wa TADB (hawapo pichani) kuhusu umuhimu wa Benki hiyo kuwafikia
wakulima wote nchini.
Afisa Tathmini wa Mikopo Mwandamizi wa
TADB, Bw. Mubezi Buberwa (kulia) na Afisa Mahusiano na Masoko Mkuu wa
TADB, Bw. Saidi Mkabakuli (wapili kulia) wakimsikiliza kwa makini Naibu
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Tate Ole Nasha (MB)
(mwenye tai) wakati alipotembelea Banda la TADB.
Afisa Tathmini wa Mikopo Mwandamizi wa
TADB, Bw. Mubezi Buberwa (kulia) akifafanua hoja mbali mbali kuhusiana
na mikopo inayotolewa na Benki hiyo.
Afisa Mahusiano na Masoko Mkuu wa TADB,
Bw. Saidi Mkabakuli (kulia) akimuelezea Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na
Uvuvi Mheshimiwa William Tate Ole Nasha (MB) (mwenye tai) mpango wa
TADB kuwafikia wakulima nchi nzima.
Na Mwandishi wetu, Bukoba
Wito umetolewa kwa Benki ya Maendeleo ya
Kilimo ya Tanzania (TADB) kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo
nchi nzima ili kuweza kuwakwamua katika changamoto zinazorudisha nyuma
juhudi zao za kujiongezea kipato kwa kukosa mitaji ya uhakika katika
kuongeza tija ya kilimo nchini.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa
Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Tate Ole Nasha (MB) wakati
akifungua rasmi Maadhimisho ya Kampeni ya Wiki ya Maziwa inayofanyika
Kitaifa mjini Bukoba, mkoani Kagera.
Mhe. Ole Nasha amesema kuwa dhima ya
kuanzishwa kwa TADB ni kutoa suluhisho la ufinyu mkubwa wa upatikanaji
wa fedha na mikopo kwa wakulima wadogo nchini ili kuchagiza maendeleo ya
kilimo nchini hivyo Benki ina wajibu wa kuwafikia wakulima wote wadogo
wenye uhitaji wa mikopo.
“Nawaomba mujielekeze kutoka mikopo yenu
ya gharama nafuu kwa wakulima wadogo ambao hawawezi kupata mikopo
kwenye benki za biashara ili kutekeleza lengo la Serikali la kuwainua
wakulima kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia
kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini,” Mhe. Ole Nasha
alisema.
Aliongeza kuwa anafahamu kuwa Serikali
ikishirikiana na TADB ilifanya mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) na kupelekea Bodi ya Benki ya Maendeleo Afrika kutoa
kibali cha kuipatia TADB fedha za kukopesha kwenye sekta ya kilimo, na
kuitaka Benki hiyo kutumia fedha hizo kwa kuwapatia wakulima wadogo
ambao ni wahitaji zaidi wa miko hiyo.
“Naomba muwakopeshe wakulima hizo fedha ya zaidi Bilioni 200 ili kuwaongezea tija katika shughuli zao,” aliongeza.
Kwa mujibu wa mpango kazi wa TADB hadi
kufikia miaka mitano ijayo itakuwa imefungua ofisi sita za kikanda zenye
lengo la kuwahudumia wakulima wote nchini. Ambapo katika hatua za awali
Benki hiyo inaendelea kuwajengea uwezo wakulima wa nchi nzima ili
kuwaandaa kupata mikopo kutoka Benki hiyo.
Mpango kazi huo unaweka bayana malengo
mengine yanayojumuisha utafutaji wa fedha toka vyanzo mbalimbali zenye
gharama nafuu kwa minajili ya kuwakopesha Wakulima katika hatua zote za
mnyororo wa ongezeko la thamani kwenye mazao ya Kilimo na kupanua wigo
wa utaoji mikopo toka Minyororo Kumi na Minne (14) ya mwanzo na
kuhusisha pia mazao mengine ya Kilimo na pia kuwaunganisha wakulima na
masoko ya ndani na nje ya nchi.
TADB ni taasisi ya serikali ambayo
ilianzishwa kwa ajili ya kutatua ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha
mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini ambao ulikuwa unachangiwa
kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa
zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa; riba kubwa kwenye mikopo ya
kilimo; mikopo ya muda mfupi; masharti magumu ya kukopa bila kuzingatia
hali halisi ya sekta ya kilimo na mazao ambayo inaathiriwa kwa kiasi
kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
No comments: