Mkuu wa Mkoa wa
Rukwa Kamishna (Mstaafu) Zelote
Stephen
RUKWA
KATIKA
kuhakikisha Mkoa wa Rukwa Upo salama kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola
yatakayoweza kujitokeza, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna (Mstaafu) Zelote
Stephen(pichani) amefanya ziara ya siku tatu katika mwambao wa ziwa Tanyangika
kwenye Kata ya Kirando, Kabwe na Kasanga vijiji ambavyo vipo jirani na nchi
ya DRC ili kujionea namna Halmashauri ya Nkasi na Kalambo zilivyojipanga
kuhakikisha kuwa ugonjwa huo hautii mguu katika Mkoa na nchi kwa ujumla.
Ziara
hiyo aliianza siku ya Ijumaa tarehe 26 hadi 28. 05. 2017 mara baada ya kumaliza
kumalizika kwa mafunzo ya siku tatu yaliyohusu utumaji wa taarifa za magonjwa
kwa kieletroniki (e-idsr) yenye kusisitiza tahadhari ya ugonjwa wa ebola uliopo
katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yaliyotolewa kwa
wahudumu wa afya wa Serikali na Sekta binafsi kwa Halmashauri mbili za Manispaa
ya Sumbawanga na Sumbawanga vijijini.
Mafunzo
ya awamu ya pili yanatarajiwa kumalizika tarehe 31. 05. 2017 kwa Halmashauri za
Kalambo na Nkasi ikiwa ni muendelezo wa awamu ya kwanza kwa Halmashauri ya
Sumbawanga Vijijini na Manispaa ya Sumbawanga yaliyoisha tarehe 26. Mwezi wa
tano.
Ili
kujiridhisha na maandalizi ya Halmashauri zinazopakana na nchi za jirani yaani
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pamoja na Zambia Mkuu wa Mkoa alipita
katika bandari maarufu za pwani ya ziwa Tanganyika na kuongea na vyombo vya
usalama ikiwemo uhamiaji, Sumatra, TRA, jeshi la polisi, jeshi la wananchi,
maafisa forodha pamoja na maafisa afya kutoka Wilayani.
Pia
Mh. Zelote aliongea na viongozi wa serikali za vijiji na kata wakiwemo
madiwani, watendaji wa kata na vijiji, wenyeviti wa vijiji na vitongoji,
maafisa ugani wa kata na vijiji, maafisa afya wa kata na vijiji na kufanya
mikutano ya hadhara ili kuwapa wananchi ujumbe aliokwenda nao katika
kuhakikisha ugonjwa huo haunusi katika mkoa wa Rukwa na nchi ya Tanzania.
Pamoja
nae Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Boniface
Kasululu, Mratibu wa Chanjo Mkoa Gwakisa Pamoja na Afisa kutoka Wizara ya Afya
wa usimamizi na ufuatiliaji Solomon Mushi, Mkuu wa Wilaya, makatibu tawala wa
wilaya pamoja na kamati za ulinzi na usalama za Wilaya.
Katika
kila Wilaya aliyopita Mh. Zelote alihakikisha anapewa taarifa za maandalizi ya
Wilaya na kisha kwenda kwenye mipaka ili kujionea kwa macho yake maandalizi
hayo na pia kuongea na wananchi wanoishi karibu na mipaka hiyo.
Wakati
akiwa kwenye ziara hiyo Mh. Zelote alikuwa akisisitiza utayari pamoja na
kujihadhari kwa viongozi wa serikali za vijiji na kata na pia kwa vyombo vya
usalama vya maeneo hayo ya mipakani.
Katika
suala la utayari Mh. Zelote Alisema kuwa wananchi wanapaswa kuelimishwa juu ya
athari ya ugonjwa huo na namna ya kujikinga nao ikiwa ni pamoja na kuelezwa
dalili za ugonjwa na njia za maambukizi ya ugonjwa huo na kuwasisitiza wananchi
kwenda zahanati pindi wanapojiskia kuumwa na sio kukimbilia kwenye maduka ya
dawa na kuagiza vidonge bila ya kujua ugonjwa anaoutibu.
Pia
katika kusisitiza hilo Mh. Zelote aliwasihi wananchi kutokimbilia kwa waganga
wa kienyeji pindi wanapoumwa na badala yake wakimbilie kwa wataalamu wa afya
kwenye zahanati ama vituo vya afya. Na kuwaonya kuwa kupitia hizi taarifa za
ugonjwa wa ebola kunaweza kukajitokeza matapeli ambao watajitangaza kuutibu
ugonjwa huo jambo ambalo si kweli, hivyo aliweka msisitizo kuwa ugonjwa wa
Ebola hauna Tiba.
“Mtu
yeyote atakayejiskia vibaya basi haraka akimbilie kwenye zahanati ama kituo cha
afya na sio kwa mganga wa kienyeji, na mjiepushe mbali sana na matapeli
wanaotibu watu vichochoroni ama wanaosema dawa ya Ebola ipo,…. Hakuna,” Mh.
Zelote alieleza.
Pamoja
na hayo Mh. Zelote alionya kuwa katika kusimamia jambo hilo hatakuwa na utani,
dhihaka ama masihara kwayeyote atakaekiuka taratibu zilizowekwa ili kujihadhari
na ugonjwa huo kuingia katika mkoa wa Rukwa.
“Mimi
nafahamu kwamba watu wanaoishi humu kwenye mipaka wameoa ama kuolewa katika
nchi za jirani, na kwamba watanzania utamaduni wetu ni ukarimu kwa wageni
lakini katika hili tupunguze ukarimu mpaka jambo hili liishe, na yeyote
atakayegundulika anamhifadhi mgeni kinyume na taratibu, huyo ni mhalifu,” Mkuu
w Mkoa alisema.
Katika
kuonesha athari kubwa inayoweza kupatikana endapo uginjwa huo utapenya katika
nchi yetu Mh. Zelote alieleza kuwa gharama za kumshughulikia mgonjwa mmoja ni
kubwa sana na kuongeza kuwa endapo ugonjwa huo unathibitishwa kwenye nchi
Fulani basi tatizo hilo si la nchi hiyo tu ni la dunia nzima.
“Nguo
inayotumika kumshughulikia mtu mmoja inauzwa milioni 10 na kwa wenzetu huko
afrika ya magharibi Ivory Coast ambako walikumbana nao watu 11,000 walifariki,
wakiwemo madaktari ambao walikuwa wakiwauguza wagonjwa, mtu mmoja tu akiupata
basi kijiji kizima kinafungwa hakuna mtu kuingia katika kijiji hicho wala
kutoka,” Mh. Zelote alisisitiza.
Lakini
pia aliwatoa hofu wananchi na kuwaambia kuwa mpaka sasa Tanzania hakuna mgonjwa
hata mmoja wa Ebola.
Nae
Daktari wa Mkoa Dkt. Kasululu alisema kuwa tangu ugonjwa huo kutolewa taarifa
na Wizara ya Afya tarehe 12. 05. 2017 watu watatu wlikuwa wamefariki na wengine
12 walikuwa wako chini ya uangalizi lakini hadi kufuikia tarehe 25. 05. 2017
idadi ya wagonjwa iliongezeka hadi kufikia wagonjwa 45 na kuongeza kuwa idadi
hiyo huenda ikaongezeka kadiri siku zinavyokwenda mbele.
“Idadi
ya wagonjwa imekuwa ikiongezeak kila kukicha hivyo ni jukumu letu kuhakikisha
tunajiandaa na kujihadhari kweli, maana wagonjwa hawa wapo kwenye misitu ambapo
usafiri wa kawaida haufiki isipokuwa Helkopta na pikipiki, hivyo wagonjwa
wanaweza kuwa wengi na bado hawajajulikana,” Dkt Kasululu alisisiza.
Nae
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Dk. Makundi Maige alielezea mikakakti ya
Halmashauri ya Nkasi namna ilivyojipaga kuhakikisha wanakaa mbali na ugonjwa hatari
wa Ebola.
“
Wilaya imeainisha kata tatu za Kirando, Kabwe na Wampembe ambazo zimetengwa
kwaajili ya kupokea wageni kutoka nchi za jirani, tukifahamu kuwa katika
mwambao wa Ziwa Tanganyia kuna Kata 10 ambazo ugonjwa huu unaweza kuingia kwa
urahisi, ambazo ni Kabwe, Kirando, Wampembe, Itete, Kipili, Mkinga, Korongwe,
Ninde, Kizumbi na Kala,” Dk. Makundi aliainisha.
Katika
kubainisha upokezi wa wageni hao Dk.
Makundi alisema kuwa kituo cha Wampembe
kitapokea wageni wanoelekea kijiji cha Kilambo hadi Msamba, Kituo cha Kirando
kitapokea wageni wanaoelekea kijiji cha Ninde hadi Kazovu na kituo cha Kabwe
kitapokea wageni wanaoelekea kijiji cha Utinta hadi Kalila.
Na
kuongeza kuwa wageni wote kutoka nchi za jirani watalazimika kupitia katika
vituo hivyo na sio kuingia kiholela kama ilivyozoeleka na kabla ya kuendelea na
safari zao watakuwa wakichunguzwa afya zao.
Kwa
kuzingatia namna ugonjwa huo unavyoenea Wilaya imetenga eneo maalum kwaajili ya
matibabu ili kuepuka kuchanganya wagonjwa watakaobainika kuwa na dalili za
ugonjwa wa Ebola.
Pamoja
na hayo Wilaya imejipaga kuzizungukia kata zote 10 na kutoa elimu kwa wananchi
na viongozi wa maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha viongozi wa dini,
wazee maarufu, vijana, waalimu na wanafunzi juu ya ugonjwa huo hatari.
Nao
upande wa Wilaya ya Kalambo walieleza mipango yao juu ya udhubiti wa
ugonjwa huu, ambapo mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Alcado mwamba aliweza uainisha
tahadhari mbalimbali ambazo Wilaya imezichukua kuhakikisha wanaudhibiti ugonjwa
huo kutokuingia katika Wilaya hiyo.
Miongoni mwa tahadhari walizochukua ikiwa ni kuwasambazia wananchi
vipeperushi vyenye kutoa elimu ya ugonjwa wa Ebola lakini pia kuihamasisha
jamii kutoa taarifa haraka kwa uongozi wa serikali pindi tu wakibaini kuna
mgeni aliyeingia kinyume na taratibu zilizowekwa.
No comments: