Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu jana aligoma kutoka katika chumba cha mahakama kufuatia kuwepo kwa tetesi kuwa kuna baadhi ya polisi wametumwa kumkamata kiongozi huyo. Lissu alifika mahakamani hapo jana asubuhi kwa ajili kusimamia
kesi ya migogoro ya ndani ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) iliyokuwa
ikisikilizwa na Hakimu Proches Mushi.
Katika kesi hiyo, Kamati ya Utendaji ya CWT wilaya imefungua
kesi dhidi ya Katibu Mkuu wa CWT, Yahaya Msulwa wakimtuhumu kwa matumizi mabaya
madaraka.
Hata hivyo wakijadili muda wa kurudi tena kwa kesi hiyo, Lissu
ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS) alisema kuna
polisi waliovalia kiraia waliokuwa wakimngojea nje ili wamkamate na
kumsafirisha kwenda Dar es Salaam.
Habari za kutaka kukamatwa kwa Lissu zilisikika asubuhi
katika mitandao ya kijamii baada ya kutumiwa ujumbe kuwa kuna maaskari
waliovalia kiraia wanataka kumkamata.
“Mheshimiwa naomba kesi hii isisomwe tarehe 23
kwa sababu sitakuwepo nchini, natarajia kwenda Uganda kwenye kikao cha vyama
vya Afrika Mashariki vya mawakili,”alisema na kuongeza:
“Lakini pia nimepewa taarifa kuwa hapo nje
kuna polisi wananisubiri nikitoka wanikamate na kunisafirisha kwenda Dar es
Salaam hivyo huenda tarehe hiyo (Julai 23) nisiwe huru kuhudhuria kesi.”
Akijibu maombi hayo Mushi alisogeza kesi hiyo hadi Septemba
27-29 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.
Mara baada ya kesi kuahirishwa, Lissu akafanya mkutano na
waandishi wa habari ndani ya ukumbi wa mahakama hiyo na kudai hatatoka
mahakamani hapo ili aone kama polisi wana uwezo wa kuingia na kumkamata.
“Leo asubuhi nimepata taarifa kutoka Dar es
Salaam kwa mama watoto wangu kwamba polisi walikuja nyumbani kwangu kunitafuta
na wakaelezwa kwamba yuko Dodoma kwa muda wa siku tatu,” alisema.
“Baada ya hapo wasamaria wema walinitaarifu
kuwa Jeshi la Polisi Dar es Salaam limewaomba wenzao wa Dodoma wanikamate pindi
tu nitakapotoka hapa na kunirejesha Dar es Salaam.”
Alipoulizwa sababu inayofanya polisi watake kumkamata, Lissu
amesema ni kutokana na maoni yake aliyoongea juzi ya kuukosoa uongozi wa Rais
Magufuli.
“Rais Magufuli na chama chake wameshindwa
siasa na wanachofanya sasa ni kutumia mabavu lakini wao kama Chadema kamwe
hawataogopa wala kukaa kimya kwani kazi yao si kumsifia Rais bali ni kumkosoa
anapofanya vibaya,”amesema.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema hakuna
sheria yoyote inayowaruhusu polisi kumkamata wakili akiwa katika shughuli zake
mahakamani.
“Nakaa nione kama watavunja sheria ya kuja
kunikamatia hapa hapa mahakamani. Nimeshazoea kukamatwa tangu mwaka huu uanze
nimekamatwa mara nne,”alisema.
Baada ya kukaa mahakamani kwa saa nne, alifika Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa na kumweleza Lissu kwamba Jeshi la Polisi
Dodoma halina taarifa yoyote wala mpango wowote wa kumkamata.
“Hatujapokea taarifa yoyote wala maelekezo
yoyote ya kukukamata kutoka makao makuu. Hata ingekuwa hivyo tungeshakukamata
kwa sababu muda wa mahakama umekwisha. Kwa sasa hivi yamebakia majengo tu kwa
hiyo uwe huru uendelee na shughuli zako,” Mambosasa alimwambia mbunge huyo.
Baada ya Mambosasa kuondoka katika mahakama hiyo, Lissu naye
aliondoka katika eneo hilo.
|
No comments: