kamanda wa polisi mkoa wa Geita Joseph konyo akiongea na mwaandishi wa habari juu ya mauaji ya sakari wanyama poli .
Bukombe
Wanakijiji wa Namonge mkoani
Geita, wameua watu wawili ambao ni askari wa wanyama pori na msaidizi
wake, baada ya kuwashambulia kwa mawe, mapanga, rungu na nondo
wakiwatuhumu kuwa ni majambazi.
Kufuatia mauaji hayo yaliyotokea wilayani Bukombe, watu 24 akiwamo ofisa mtendaji wa kijiji hicho wanashikiliwa na polisi.
Tukio hilo limetokea juzi jioni baada ya wananchi hao kukusanyana na kuivunja ofisi ya serikali ya kijiji hicho ambako walinzi hao walikuwa wamehifadhiwa na ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Andrea Malise.
Malise aliwaweka kwenye ofisi hizo wakati akifanya jitihada za kuwasiliana na polisi wafike eneo la tukio kuwaokoa.
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Amani Mwenegoha, akisimulia tukio hilo alisema hadi jana watu 24 akiwamo Mali wanashikiliwa kwa tuhuma hizo na uchunguzi unaendelea.
Wananchi walioshuhudia mauaji walisema juzi alasiri watu watano, mmoja wao akiwa na silaha aina ya SMG walipita kijijini baadaye kuingia baa wakiwa na pikipiki lakini safari hiyo bila silaha. Kutokana na kuonekana wageni wanakijiji walianza kuhoji na kuwasiliana juu ya wageni hao.
Pasipo subira inadaiwa wananchi walianza kuwatupia mawe na kuwashambulia ndipo ofisa mtendaji alipoingilia kati na kuwaweka katika ofisi yake kukwepa vipigo kutoka kwa wananchi hao.
Aliwafungia na kuwasiliana na polisi wa kituo cha Lunzewe kilichopo umbali wa kilometa 30 na kabla hawajafika wananchi walianza kuwashambulia na kubomoa jengo la ofisi kuvunja milango na madirisha na kuingia ndani.
Baada ya kulivunja jengo la ofisi ya serikali ya kijiji, waliwashambulia hadi kuwaua na kisha kuchukua kila kitu walichokuwa nacho zikiwamo fedha mifukoni, kuiharibu pikipiki yao na kugawana vifaa vyake zikiwamo tairi na taa kabla ya polisi kufika eneo hilo.
Hofu ya wananchi inadaiwa inachangiwa na kuwapo kwa matukio ya kihalifu ya mara kwa mara katika ukanda huo, likiwamo la mnada wa ng'ombe kuvamiwa na watu wenye silaha Januari 16 mwaka huu na wengine wenye silaha kuingia katika kijiji cha Ilyamchele siku tatu baadaye na kuwateka wanakijiji baada ya kuwakirimu.
Pamoja na kuwapo mazingira na utetezi huo imedaiwa kuwa serikali isipochukua hatua kali kukomesha uchukuaji sheria mikononi, ipo hatari ya kuibuka tabia ya kulipizana kisasi na kubambikiziana tuhuma na hivyo kukosekana kwa utawala wa sheria na kikatiba na kuuawa kwa watu wasio na hatia.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Namonge Charles John, alithibitisha kuwa waliuawa baada ya ofisi ya serikali ya kijijiji kuvunjwa na kwamba marehemu hao walitambuliwa na askari wenzao wa wanyamapori.
No comments: