Makaburi 5 yakijegelewa ktk kijiji cha Bugalama Maswa baada ya familia
moja kuuawa kwa kukatwakatwa mapanga-Picha na Samweli Mwanga- Simiyu
Nyumba aliyokuwa akiishi marehemu George Charles ktk kijiji cha Bugalama
Maswa kabla ya kuuawa kwa kukatwa mapanga yeye na familia yake akiwemo
mke na watoto watatu-Picha na Samweli Mwanga- Simiyu
Katika hali isiyokuwa ya kawaida watu watano wamefariki dunia papo hapo
kwa kukatwa katwa mapanga kama wanyama katika kitongoji cha Kisesa kata
ya Bugalama wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu.
Watu hao ambao ni wa familia moja walifanyiwa unyama huo kwa kukatwa
katwa mapanga sehemu ya shingoni, huku wahusika wa tukio hilo wakiwa
hawajajulikana.
Akitoa taarifa mbele za waandishi wa habari Kamanda wa polisi Mkoani
hapa Gemine Mushy alisema tukio hilo lilitokea jana ambapo Baba, Mama
pamoja na watoto wao 3 ndiyo waliouawa.
Mushy aliwataja waliofanyiwa unyama huo kuwa George Charles (30) ambaye
ni Baba wa familia, Siku John (23) Mama wa Familia na watoto wao ambao
ni Mchambi George (7) Tuma George (5) pamoja na Amos George (Miezi 9)
wote wasukuma wa kitongoji hicho.
Aidha Kamanda Mushy alieleza chanzo kuwa ni mgogoro wa ardhi kati ya
marehemu (George) pamoja na Baba yake wa kambo ambaye alinunua kipande
cha ardhi alikokuwa akiishi marehemu.
Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo jeshi la polisi lilifanya msako na
kuwakamata watuhumiwa 3 ambao aliwataja kuwa ni Migata Lusalago (50)
Jihelya Migata (30), Solo Kengele (31) wote wasukuma wa kijiji cha
Bugalama.
Kamanda mushy alieleza kuwa waliokamatwa ni Baba wa kambo wa Marehemu
pamoja na watoto wake wawili ambao ilidaiwa kuwa wameweza kushiriki
katika kutenda tukio hilo la kinyama.
Hata hivyo Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa uchunguzi wa kina unaendelea
kufanyika ili kuwapata wahusika zaidi wa tukio hilo, ambapo aliwataka
wananchi kutoa ushirikiano katika kudhibiti uhalifu ususani mauaji
yatokanayo na ukataji wa mapanga.
No comments: