*Jenerali
Mwamunyange atangaza msako usiku,mchana,
SERIKALI
imetuma kikosi maalumu cha ulinzi, kikiongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kuwasaka watu wanaodaiwa kuwa majambazi ambao
wanaendesha mauaji ya kinyama mkoani Tanga.
Uamuzi huo
umechukuliwa baada ya watu wanane kuuawa kinyama kwa kuchinjwa juzi usiku
katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, Manispaa ya Tanga.
Habari za
uhakika ambazo MTANZANIA imezipata jana, zinasema tayari vikosi hivyo vimeanza
operesheni kali katika mapango ya Amboni ambayo yanadaiwa kuwa maficho ya watu
hao.
Akitoa
salamu za rambirambi wakati wa mazishi ya marehemu wanne kati ya wanane
waliozikwa Kibatini jana, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis
Mwamunyange, alisema vyombo vya dola vitahakikisha watu wote waliohusika katika
mauaji hayo wanatiwa mbaroni.
“Ndugu
zangu nawapeni pole kutokana na kuondokewa na wapendwa wetu… naomba
kuwahakikisha sisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola tutahakikisha
tunawatia nguvuni watu wote waliohusika na mauaji haya,” alisema Jenerali
Mwamunyange.
Alisema
tukio la mauaji hayo ni la kusikitisha mno kutokana na Tanzania kusifika kuwa
nchi ya amani duniani.
“Tanzania
inasifika kuwa na amani duniani kote, lazima hatua za kiusalama zichukuliwe
haraka ili kunusuru amani yetu isichezewe.
“Ni tukio
la ajabu ambalo limegusa watu wengi wasio na hatia, tutasaidiana na wenzetu
kuhakikisha wahalifu hawa wanapatikana,” alisema Jenerali Mwamunyange.
WAZIRI MASAUNI
Naye Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni Hamad Masauni, alisema Serikali
inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo ili kuwakamata wahusika ndani ya
kipindi kifupi.
Aliwahakikisha
wananchi kuwa ulinzi unaimarishwa na kwamba matukio hayo hayatajirudia tena.
“Vyombo
vya ulinzi vitafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha tunawatia nguvuni
haraka watu waliohusika na mauaji hayo,” alisema Masauni.
Aliwaomba
ndugu na jamaa ambao wamefiwa na ndugu zao kuwa na subira wakati Serikali
inaendelea kuchukua hatua.
Naye Mkuu
wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu alisema wataendelea kuimarisha ulinzi na
usalama maeneo yote.
WANANCHI
Katika
hatua nyingine, wakazi wa mitaa mitatu ya Mleni Kati, Mleni Mashariki na
Kibatini katika Kata ya Mzizima, Manispaa ya Tanga, wameanza kukimbia makazi
yao kwa kuhofia usalama wao baada ya mauaji hayo.
Mauaji
hayo yalitokea juzi usiku ambapo watu wanaoaminika kuwa majambazi walivamia
nyumba tatu katika eneo hilo, wakiwa wamelala usiku, kisha kuwateka na
kuwapeleka msituni kabla ya kuwachinja.
Wakazi hao
wanaounda zaidi ya kaya 30, walisema wameamua kuyakimbia makazi yao kwa
kutokuwa na imani ya usalama wao katika eneo hilo, baada ya wale wanaoitwa
majamabzi kuvamia makazi yao kwa mara ya pili kwa staili ya kutisha.
Kabla ya
tukio hilo la juzi, watu wasiofahamika walivamia makazi yao na kuchinja kuku
40, mbuzi wanne na ng’ombe mmoja na kukimbilia mapango ya Amboni na hawajawahi
kukamatwa.
MTANZANIA
jana lilishuhudia wanawake na watoto wakiwa na mizigo mithili ya wakimbizi
wakiondoka katika eneo hilo huku wanaume wakibaki kwa ajili ya kuzika ndugu,
jamaa na marafiki zao waliouawa katika tukio hilo.
Mmoja wa
wananchi hao, Juma Issa, alisema wamelazimika kuwahamisha wanawake na watoto
kwa kuhofia wanaweza kuvamiwa tena kwa mara ya pili.
Nae Lucas
Muhina alisema kuwa anashindwa kuhama katika eneo hilo kutokana na kuwa na
mifugo, hivyo anashindwa kujua mahali salama pa kuihifadhi.
Mwenyekiti
wa Kitongoji cha Kibatini, Shabani Mwamini, alithibitisha baadhi ya
wananchi wa mitaa mitatu kuhama katika eneo hilo.
“Nyumba
nyingi zimebaki na wanaume pekee yake kwani wanawake na watoto wote wamehama
kwa sasa,” alisema.
Wakati
huohuo, maiti nne kati ya nane zimezikwa jana huku nyingine nne zikisafirishwa
nje ya mkoa huo.
Mwamini
aliwataja waliozikwa kuwa ni Issa Husein, Mkola Husein, Issa Hamis
na Salim
Adam.
Mkuu wa
Mkoa wa Tanga, Martin Shigella alisema kuwa vyombo vya dola vinaendelea na
uchunguzi kuhusu tukio hilo.
SIMULIZI ZA MAUAJI
Mtoto wa marehemu Mkola Hussein
anayeitwa Salimu Mkola (16) alisababisha vilio na simanzi kwa waombolezaji baada ya kusimulia namna watu hao walivyomchukua baba yake na kwenda kumchinja mbele ya nyumba yake.
anayeitwa Salimu Mkola (16) alisababisha vilio na simanzi kwa waombolezaji baada ya kusimulia namna watu hao walivyomchukua baba yake na kwenda kumchinja mbele ya nyumba yake.
Akisimulia
tukio hilo huku akibubujikwa machozi, mtoto huyo alisema watu hao walifika
nyumbani kwao wakagonga mlango saa sita usiku na kumuamrisha baba yao atoke na
fedha.
“Nilipoona hivyo nilijaribu kupiga kelele
kuomba msaada kwa majirani, lakini mmoja wa wauaji aliingia ndani na kunitoa nje ya nyumba yetu, huku akiniuliza wakati wale vijana saba
wanachukuliwa na polisi mimi nilikuwa wapi.
kuomba msaada kwa majirani, lakini mmoja wa wauaji aliingia ndani na kunitoa nje ya nyumba yetu, huku akiniuliza wakati wale vijana saba
wanachukuliwa na polisi mimi nilikuwa wapi.
“Waliendelea kuniuliza kama nina habari ninayoijua, huku wakiwa
wameshika mapanga na bunduki, ndipo waliponiambia wapo kwa ajili ya kutetea
dini yetu.
“Baadaye waliniruhusu niingie ndani na kulala, lakini niliendelea kusikia vishindo vya kipigo na watu wakikoroma ambayo ilikuwa ni ishara ya kuwa baba yangu alikuwa anakata roho pamoja na watu wengine,” alisema.
Mtoto mkubwa wa marehemu, Abuu Mkola, alisema vijana saba ambao sasa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi awali walionekana katika Kitongoji cha Kibatini wakiwa wanakimbia kusikojulikana.
Alisema baada ya hali hiyo baba yake ambaye ni marehemu, Mkola
Hussein
akishirikiana na wananchi wa mtaa huo walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao walikuja na kuwakamata vijana hao lakini mmoja wao alifanikiwa kukimbia.
akishirikiana na wananchi wa mtaa huo walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao walikuja na kuwakamata vijana hao lakini mmoja wao alifanikiwa kukimbia.
Abuu alisema kuwa katika tukio la juzi, wauaji hao wakati wanamchukua baba yake walisema wanawahitaji vijana wao saba waliokamatwa na polisi, lakini aliposema hajui ndipo walimuunganisha na watu wengine kwa ajili ya kumchinja.
BUNGENI
Ofisi ya
Bunge imeiagiza Serikali kutoa taarifa rasmi kuhusu mauaji yanayoendelea nchini
ili kuwatoa hofu wananchi waliopo katika maeneo mbalimbali.
Akitoa
maagizo hayo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alisema Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni anapaswa kuzungumza na Kamati za Ulinzi na
Usalama katika maeneo yote ambayo yametokea mauaji ili aweze kutoa taarifa
ndani ya Bunge.
“Waziri
atuletee taarifa kwa sababu Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) yupo hapa na
waziri anayehusika na mambo ya Bunge yupo, naomba watuletee taarifa kwa sababu
mauaji yamekuwa yakitokea mara nyingi na tumekuwa tukiwasihi Serikali
ituletee taarifa na si mtakuwa mnazitafuta,” alisema Dk. Tulia.
Baada ya
maelezo hayo Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisimama na kuomba mwongozo
chini ya kanuni 68 (7).
“Mheshimiwa
Naibu Spika pamoja na haya uliyoyatolea maelezo juu ya mauaji yanayotokea
katika nchi yetu, nimelazimika kuomba mwongozo huu kwa sababu matukio
yaliyoanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali na maeneo mengine
mambo haya tuliwahi kuyauliza Serikali na kuahidi watayatolea ufafanuzi.
“Sasa
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani amekwenda kuangalia na atazungumzia
jambo hilo wakati mambo haya wabunge tulishaiomba Serikali itoe ufafanuzi ni
jinsi gani inajipanga kukabiliana nayo,” alisema Lugola.
Alisema
kitendo cha Serikali kusema Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amekwenda
kushughulikia jambo hilo wakati huo huo mambo ambayo yametokea Mwanza na maeneo
mengine yalishaombewa ufafanuzi lakini hakuna majibu si kizuri.
CUF WATAKA UKWELI
Chama cha
Wananchi (CUF) kimelaani mauaji hayo.
Katika
taarifa iliyotolewa jana kwenye vyombo vya habari na kusainiwa na Naibu
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Abdul Kambaya, ilisema
vitendo hivyo katika Jiji la Tanga si mara ya kwanza kutokea.
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, CUF imelitaka Jeshi la Polisi kuwaeleza Watanzania ukweli wa
tukio hilo na mengine kama hayo kabla taasisi na mashirika mengine binafsi
hayajatoa ukweli wa suala hilo.
Kwa hisani ya gazeti la mtanzania
No comments: