WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa Daraja la waenda kwa miguu lililopo eneo la Furahisha na barabara ya kutoka Furahisha hadi Pasiansi yenye urefu wa KM 2.7, imekamilka kwa asilimia 99 Mkoani Mwanza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongela (kulia), wakishuka ngazi za daraja la waenda kwa miguu lililojengwa eneo la Furahisha, alipokagua ujenzi wake mkoani Mwanza.
Mhandisi Mkazi anayesimamia uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Mwanza Bw. Geofrey Asulumenye, akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, upanuzi wa njia za kurukia ndege katika kiwanja hicho mkoani humo.
MWANZA
Prof. Mbarawa amesema hayo wakati alipokuwa
akikagua maendeleo ya ujezi wa daraja hilo katika ziara yake ya kikazi mkoani
humo na kuridhishwa na ukamilishwaji wa ujenzi wake.
“Daraja hili litaondoa changamoto kwa wananchi
wanaotembea kwa miguu na litapunguza au kuondoa adha ya msongamano wanaovuka
kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amewataka wananchi kutunza
daraja hilo na miundombinu yake ili liweze kutumika kwa muda mrefu kwani
limekuwa nembo ya Mkoa wa Mwanza.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John
Mongela, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
kwa kujenga Daraja la Furahisha kwa kuwa limebadilisha mandhari ya Jiji hilo.
“Jiji la Mwanza ni kitovu cha Kanda ya Ziwa,
wananchi wameguswa moja kwa moja na mradi wa ujenzi wa daraja hili”, amesema . Mongela.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara
Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mwanza, Eng. Marwa Rubirya amemweleza Prof.
Mbarawa kuwa kazi iliyobaki katika daraja hilo nikuweka taa za urembo.
Ameongeza kuwa Daraja hilo pamoja na barabara
yake zimegharimu kiasi cha zaidi ya cha shilingi Bilioni nne na linatarajiwa
kuanza kutumika ndani ya siku mbili zijazo.
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa amekagua
upanuzi wa barabara ya Makongoro hadi Uwanja wa Ndege wenye urefu wa KM 5.3,
ambapo malipo ya awali yameshalipwa kwa mkandarasi na mradi unatarajiwa
kukamilika mapema kabla ya muda ambao umepangwa mwezi Mei mwakani.
Prof. Mbarawa amekagua uboreshaji wa kiwanja
cha ndege cha Mwanza ambao umehusisha ujenzi wa jengo la mizigo, barabara za
njia za ndege, jengo maalum la kuongozea ndege (Control Tower)na
upanuzi wa urefu wa uwanja hadi kufikia KM 3.8 na kuagiza TANROADS kusimamia
uboreshaji wa kiwanja hicho ili kikamilike kwa wakati uliopangwa.
Amesema kuwa hatua inayofuata ni kujenga jengo
la kisasa la abiria lenye hadhi ya kimataifa ambalo litachukua na hadhi ya
kiwanja hicho.
Uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini ni moja
ya mkakati wa Serikali katika kukuza sekta ya usafiri wa anga na kuongeza pato
la Taifa.
No comments: