Kahama
18, 2013.
UONGOZI wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA)Wilaya ya Kahama juzi umekemea vikali tabia iliyofanywa na
Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa Wilaya la kula Rushwa ili kuwatoa wanachama
wa chama hicho waliokuwa wamekamatwa na kuwekwa mahabusu kwa tuhuma za kuwazuia
watumishi wa Serikali kufanya kazi.
Akiongea mbele ya Waandishi wa habari
mjini Kahama Mwenyekiti wa baraza la vijana la Chadema ( BAVICHA) Benedict
Shija alisema kuwa kitendo kilichofanywa na Mwenyekiti wa Baraza hilo
Juma Protasi la kupokea Rushwa ya shilingi 75,000 kutoka kwa ndugu wa
watuhumiwa ni cha kulaaniwa vikali na kinyume cha katiba ya chama hicho.
Alisema kuwa sakata la kukamatwa na
Rushwa kwa kiongozi huyo lilikuja baada ya kukamatwa watuhumiwa Elias Mayunga
ambaye ni Mwenyekiti wa Chama hicho kata ya Kilago pamoja na Katibu wake Daniel
Makoye ambao walikuwa wakishikiliwa na Jeshi la polisi kwa makosa ya kuwazuia
maafisa wa Serikali kufanya kazi zao katika kata hiyo.
Alisema kuwa kufuatia Watuhumiwa
kukamatwa na kukaa mahabusu kwa muda wa siku 14 ndipo Mwenyekiti huyo
alipowafuta ndugu wa watuhumiwa hao na kuomba kiasi hicho cha fedha ili aweze
kuwatoa Mahabusu watumiwa hao huku yeye akihaidi kuongeza kiasi cha shilingi
40,000 kama kuwaunga mkono wanachama wake katika kufanikisha dhamana yao
Mahakamani.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo baada ya
kupokea kiasi hicho cha fedha Juma Protasi aliamua kuzila fedha hizo huku
akidai kuwa watuhumiwa hao wangetoka siku inayofuata hali ambayo
haikuweza kutekelezeka na ndipo baadhi ya wanachama wa Chadema Jimbo la Kahama
walipoamua kuingilia kati suala hilo hilo huku wakimtaka kurudisha fedha hizo
kwa wahusika kwani dhamana ya watuhumiwa hao ilikuwa haihitaji fedha
yeyote.
Shija alisema kuwa baada ya wanachama
kuchachamaa ndipo Mwenyekiti huyo alipoamua kufuata fedha hizo nyumbani kwake
na kufanikiwa kurudisha kiasi cha shilingi 70,000 kati ya 75,000 alizochukua
hali ambayo ilifanya wanachama hao kufikisha suala hilo katika taasisi ya kuzua
na kupambana na Rushwa (PCCB).
Kwa upande wake Mwenyekiti huyo Juma
Protasi alipotafutwa na Waandishi wa habari kwa ajili ya kuthibisha tukio hilo
hakuweza kupatikana na hata alipopigiwa simu ya kiganjani simu yake ilikuwa
ikiiita bila ya kuwa na majibu yeyote.
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la
Kahama Barikiel Israel alisema kuwa kwa sasa wanajiandaa kuitisha Kikao cha
Kamati tendaji ya jimbo kwa ajili kujadili suala hilo kabla ya kulifikisha
katika uongozi wa Mkoa kwa hatua za kinidhamu zaidi.
Pia alitoa wito kwa Viongozi wa Chama
hicho wasiwe na tamaa bali wafanye kazi kwa kufuata katiba ya Chadema kwani
chama hicho kina sera ya kupinga Rushwa na sii kuona viongozi wake wanakuwa
katika mastari wa mbele katika kula Rushwa tena kwa wanachama wake wenyewe.
Mwisho.
No comments: